Jumamosi mwanasosholaiti maarufu kutoka Uganda Zari Hassan alitimba nchini Tanzania akitokea Afrika Kusini kwa ajili ya kuongoza kipindi cha uhalisia katika nchi hiyo ambayo alikuwa ameolewa na mwanamuziki Diamond Platnumz kabla ya kuachana miaka 6 iliyopita.
Zari alirejea wiki moja tu baada ya kuvuma mitandaoni kwa kutupiana maneno ya nguoni na mwanasosholaiti kutoka Ghana, Fantana ambaye alionekana akimbusu kwa mahaba Diamond Platnumz katika kipindi cha uhalisia kwenye Netflix cha Young, Famous & African.
Zari alianzisha ugomvi mkali na Fantana lakini pia akimlipua vikali Diamond kwa kile alisema kuwa msanii huyo alikwenda kudanganya waziwazi kwamba mjasiriamali huyo wa Uganda alikuwa anambembeleza kupata mtoto wa tatu naye.
Safari hii baada ya kurejea Tanzania akiwa ameandamana na mpenzi wake Shakib Lutaaya, Zari alipata fursa ya kuzungumzia harusi yao ya Nikkah ambayo ilifanyika mwezi jana, Zari aliwashangaza wengi alipofichua kwamba mpenzi wake alimpa tu Qur’an kama mahari.
Mjasiriamali huyo ambaye wakati wa kumlipua Diamond alijitaja kuwa bilionea aliyejitengeneza mwenyewe bila kushikwa mkono na mtu yeyote mwenye ushawishi, alisema kuwa ni yeye mwenyewe aliomba Shakib kumpa Qur’an na hakuwa anataka kumsumbua, kwani anataka kusongeza Zaidi maisha yake kwa Allah – Mungu kwa Waislamu.
“Bila kumpa shida nyingi, nimepata kila kitu ambacho nimewahi kutaka katika ulimwengu huu. Mungu amenibariki kwa maisha mazuri, watoto wangu wako sawa, na biashara yangu inastawi. Kwangu mimi, nilimwomba mume wangu tu Qur’an kwa sababu ninajaribu kuendeleza maisha yangu Katika Imani. Mimi pia ni Muislamu, na hata alishangaa nilipomwambia hivyo,” Zari alifunguka kwa mshangao wa wengi.
Hata hivyo, mama huyo wa watoto watano kutoka kwa baba tofauti hakufunguka iwapo anatarajia kumzalia Shakib mtoto baada ya kukamilika kwa ndoa yao.
Zari amekuwa akisutwa vikali tangu mwaka jana alipoweka wazi kwamba anatoka kimapenzi na kijana huyo ambaye anatajwa kuwa mdogo kiumri mwa mwanasosholaiti huyo.
Hata hivyo, Zari aliwanyamazisha waliokuwa wanamsuta akisema kuwa kila mtu anafaa kuzingatia maisha yake tu na kumuacha ajifurahishe na ya kwake, huku pia akitupa dongo kwa jamii ambayo kwa miaka mingi imekuwa ikiona ni hatia kwa mwanamke kutoka kimapenzi na mwanaume mdogo kiumri hali ya kuwa ni sawa kwa mwanamume mkubwa kutoka kimapenzi na mrembo mdogo kiumri.