Betty Kyallo afunguka kuhusu kilichovunja ndoa yake na Dennis Okari miezi 6 tu baada ya harusi

"Sio lazima kwa sababu niko na mtu hapa tutakuwa pamoja kwa miaka mia nyingine," Betty alisema.

Muhtasari

•Betty Kyallo amesema bado haelewi hali iliyopelekea kuvunjika kwa ndoa yake na  Dennis Okari takriban miaka saba iliyopita.

•"Kuna wengine husema hawakuwa na simu 2015. Ananiambia hongera sasa baada ya kuendelea na maisha," Betty alisema.

Dennis Okari na aliyekuwa mkewe Betty Kyallo
Dennis Okari na aliyekuwa mkewe Betty Kyallo
Image: HISANI

Mwanahabari Betty Kyallo amefichua kwamba bado haelewi hali iliyopelekea kuvunjika kwa ndoa yake na mwanahabari mwenzake Dennis Okari takriban miaka saba iliyopita.

Ndoa ya Betty na Okari ilisambaratika mwaka wa 2016, takriban nusu mwaka tu baada ya kufunga pingu za maisha katika harusi ya kufana iliyofanyika jijini Nairobi. Wawili hao walikuwa wamechumbiana kwa takriban miaka minne kabla ya harusi.

Akiongea kwenye Wicked Edition kwenye NTV, Betty alisema hajui ni nini kilikuja na harusi ambacho kilifanya ndoa yao kuvunjika.

“Ni kitu ambacho mimi bado hushangaa. Enyewe sijui iliendaje. Nadhani kuna shida tu na hiyo gauni nyeupe,” alisema.

Aliongeza,“Inaweza kuwa chochote. Lakini mimi naamini kama haingewezekana, haiwezi. Huwezi kulazimisha kitu.”

Mfanyibiashara huyo mwenye umri wa miaka 34 alibainisha kuwa yeye na mzazi mwenzake Okari sasa tayari wameendelea kimaisha na wote wana furaha katika nafasi yao mpya.

"Sio lazima kwa sababu niko na mtu hapa tutakuwa pamoja kwa miaka mia nyingine," alisema.

Hata hivyo alibainisha kuwa baadhi ya Wakenya bado hawajasahau kuhusu ndoa yao ya muda mfupi ambayo haikudumu.

"Kuna wengine husema hawakuwa na simu 2015. Ananiambia hongera sasa baada ya kuendelea na maisha," alisema.

Kyallo na Okari walichumbiana kwa takriban miaka minne kabla ya kufunga ndoa katika harusi ya kupendeza mnamo Oktoba 2, 2015 katika bustani la Marula Manor, mtaa wa Karen, Nairobi. Kwa bahati mbaya, wanahabari hao wawili waliamua kutengana na kwenda njia tofauti takriban miezi sita tu baadaye na kuwaacha Wakenya wengi katika mshtuko mkubwa.

Wakati wakichumbiana, wawili hao walibarikiwa na binti mzuri pamoja, Ivanna ambaye sasa wanashirikiana kumlea.

Mwaka jana, Betty Kyallo aliweka wazi kwamba hakuna uhasama wowote kati yake na mzazi mwenzake Dennis Okari.

Betty alifichua kwamba kuna ushirikiano mzuri kati yake na Okari katika malezi ya binti yao wa miaka minane, Ivanna.

"Kushirikiana katika malezi kumekuwa kuzuri. Ivanna anampenda sana babake na babake vilevile anampenda," Betty alisema akiwa kwenye mahojiano na Citizen Digital.

Mtangazaji huyo hata hivyo alikiri kwamba ilichukua muda kabla yao kuweza kushirikiana vizuri baada ya ndoa yao kugonga ukuta.

Alifichua kwamba kila mmoja wao huwa anapata muda wa kukaa na binti yao na huwa wanahudhuria mikutano yake shuleni pamoja.

"Huwa tunaenda na Dennis kwenye mikutano yote ya shule. Jinsi huwa tunaketi watu wanaweza kufikiri bado tuko pamoja. Hatuna ugomvi. Sisi ni marafiki. Huwa tunapigiana simu kila wakati kuhusiana na binti yetu," Alisema.