Tangu walipotangaza kuchukua likizo ya kimuziki kutoka katika kundi lao mwezi jana, Sauti Sol wamekuwa wakinukuliwa visivyo na sahihi kwa wakati mmoja kuhusu tangazo hilo.
Savara, mmoja wa wanabendi hao ambao wamekuwa wakifanya muziki kama kundi moja kwa Zaidi ya miaka 10 amefunguka na kunyoosha maelezo kuhusu tangazo hilo ambalo limevutia maoni mtanange kutoka kwa pande zote za mashabiki wao.
Akijibu swali hilo kwa mara nyingine, na pengine ya mwisho kabisa katika mkutano na wanahabari katika maandalizi kelekea siku kubwa ya tamasha la Stanbic Yetu litakalofanyika kwenye uwanja wa Uhuru Gardens jijini Nairobi mnamo Juni 10, Savara alisema kuwa hawaachi muziki kama ambavyo wamekuwa wakinukuliwa bali ni kutengana tu ili kila mmoja aweze kujitambua kibinafsi kwenye ubora wake.
“Imekuwa ni safari ya kukumbukwa, miaka Zaidi ya 15 na imefikia mahali tunahisi kwamba kila mtu anafaa kujisimamia. Si eti tunaacha muziki, ni kutengana tu tumetengana. Mtuelewe vizuri hapo kwa sababu kumekuwa na machapisho ya kupotosha kuhusu hilo,” Savara alisema.
Msanii huyo alisema kuwa biashara zingine zote ambazo zimesajiliwa kwa jina la kikundi cha Sauti Sol zitaendelea jinsi zilivyo bila kuhitilafiwa na utengano wao.
Biashara hizo ni pamoja na lebo ya Sol Generation na pia Sol Kids.
“Ni mapumziko kidogo kama ambavyo tulisema, na kila kitu kitaendelea kawaida,” Savara alisema.
Kundi hilo litatumbuiza katika kile kinatajwa kuwa kuonekana kwao pamoja kwa mara ya mwisho katika tamasha la Stanbic Yetu kabla ya kukaribisha kundi la Boyz II Men jukwaani usiku wa Juni 10.