Afisa mkuu mtendaji wa baraza la hakimiliki za muziki Kenya (MCK), Ezekiel Mutua amekashifu vikali wimbo wa msanii wa Gengetone Ssaru 'Kaskie Vibaya Huko Kwenu'.
Akizungumza katika taarifa na runinga za mitandaoni, Ezekiel Mutua alisema kuwa wimbo wake Ssaru hauna ujumbe unaoweza kusikilizwa na kizazi kichanga na ujumbe huo unawapoteza watoto kimaadili.
"Mliskia wimbo wa binti huyo akimwimbia mchumba wake wa zamani kuwa sasa yuko katika mahusiano na baba yake, 'niko na pesa na niza baba yako nenda ukasikia vibaya na huko'. kusema ukweli mnaambia nini binti yangu"
Ezekiel alisema kuwa angependa wasanii waangazie na wafanye muziki ambao unawahimiza watu kufanya vitu zinazokubalika kimaadili.
"Ni muhimu wasanii kufahamu kuwa wanaweza kutumia muziki kukuza maadili katika jamii zetu, tunaweza tumia muziki kuleta amani na uhiano baina ya watu duniani."
Ezekiel aliendeleza mashambulizi yake kwa wanamuziki wa injili kwa kile anachohisi ni kuwa wasanii hao wanazembea katika kuwaburudisha wasikilizaji na mashabiki wao.
"Ninawakosoa sana wasanii wa nyimbo za injili kwa sana kwa sababu ni sawa kwa wanamuziki wa nyimbo za kidunia kuimba nyimbo kama hizo, lakini ninatarajia wasanii wa injili kufanya muziki unaowazungumzia watu kukuza amani."
Alhamisi, Ezekiel alisema kuwa wasanii wa nyimbo za injili wamemsababishia uchungu mkubwa katika juhudi zake za kufufua sekta ya muziki nchini Kenya.
"Tangu nijiunge na MCK mwaka mmoja uliopita, watu ambao wamenipa maumivu zaidi katika juhudi zangu za kufufua sekta ya muziki nchini ni wasanii wa nyimbo za injili."
Ezekiel alikiri kuwa katika muda wa mwaka mmoja akihudumu kama afisa mkuu mtendaji wa MCK ameweza kuthibitisha madai yaliyotolewa na mchekeshaji Erick Omondi hapo awali.
"Nafikiria Erick Omondi alikuwa sawa akisema kuwa kuna kitu ambacho hakiko sawa na wasanii wa nyimbo za injili"
Kulingana naye tasnia hii ina waigizaji wengi na wasanii halisi wa injili ni wachache.