Mtangazaji wa kipindi cha asubuhi katika kituo cha Radio Jambo, Gidi Ogidi amejitapa kuwa miongoni mwa watumizi wa kwanza kabisa kujiunga katika mtandao mpya wa Threads.
Mapema wiki jana, Mmiliki wa Meta ambayo ni mzazi wa kampuni ya Facebook, Instagram na WhatsApp, Mark Zuckerburg alitangaza ujio wa mtandao mpya – Threads ambao utakuwa unatoa ushindani moja kwa moja na jukwaa la Twitter amablo linamilikiwa na tajiri namba moja duniani, Elon Musk.
Kupitia ukurasa wake wa Facebook, Gidi alijipiga kifua akisema kuwa kwa mara ya kwanza tangu ujio wa mitandao ya kijamii, amekuwa miongoni mwa watu wa kwanza kabisa kujiunga kwenye mtandao huo.
Mtangazaji huyo aliwataka mashabiki na wafuasi wake kumfuata kwenye mtandao huo mpya huku akiwapa jina ambalo analitumia kule.
“Kwa mara ya kwanza nimejiunga na jukwaa jipya la mtandao wa kijamii kama ndege wa mapema, niko kwenye THREADS 🙌 nifuate @gidiogidi,” aliandika mtangazaji huyo.
Jarida la BBC linaripoti kwamba Threads utakuwa mtandao kama Twitter lakini unaomilikiwa na mshindani wa Musk, Zuckerburg.
Mmiliki huyo wa Meta alitangaza ujio wa mtandao huo ikiwa ni siku kadhaa baada ya Musk kufanyia marekebisho kadha wa kadha mtandao wa Twitter, hatua ambayo wengi wanahisi imefifisha dhumni halisi la mtandao huo ambao kwa miaka mingi umetajwa kuwa mkubwa.
Wiki jana, Musk alitangaza kupunguza idadi ya tweets ambazo mtu anaweza kuona kwa siku, athari kubwa ikiwa kwa wale wanaojiunga upya na wale ambao akaunti zao hazijadhibitishwa kwa alama ya buluu – ambayo ni ya kulipiwa kwa ada ya dola nane kila mwezi.