Mchekeshaji David Oyando almaarufu Mulamwah amesema hana uhakika kama rafiki yake wa karibu Ruth K ni mjamzito kama ambavyo Wakenya wamekuwa wakikisia.
Katika mahojiano na wanahabari, baba huyo wa binti mmoja alifichua kwamba bado hajapata dokezo lolote kwamba Ruth anatarajia mtoto wake wa kwanza.
“Mimi sijui, mimi sijui, mimi siwezi kutarajia mtoto, ningekuwa nimesikia akigonga kwa tumbo. Lakini nitamuuliza,” Mulamwah alisema.
Mchekeshaji huyo alishikilia kuwa mrembo huyo ambaye amekuwa akiigiza naye video za burudani ni rafiki yake tu na hakuna uhusiano wa kimapenzi kati yao.
Kuhusu tetesi za kumtunga ujauzito mwigizaji huyo, alisema kuwa huenda mlimbwende huyo na mpenzi wake wameamua kupata mtoto.
“Sijajua. Mimi nitamuuliza. Labda wameamua na mpenzi wake, sijui,” alisema.
Aliongeza, “Mimi huwaambia ako na chali yake kwa hivyo maisha yake siwezi kuingilia, labda mimi niulize kama nyinyi, jambo ambalo sio sahihi kwangu kufanya. Kama ni kitu atataka tujue basi bila shaka atatuambia.”
Kwa upande wake, Mulamwah aliweka wazi kuwa bado yuko sokoni kwani kwa sasa hana uhusiano wa kimapenzi na mtu yeyote.
Alisisitiza kuwa Ruth ni mmoja wa wasanii wake na kusema huwa anaonekana sana naye kwa sababu kawaida wanafanya kazi pamoja.
Mwezi uliopita, muigizaji Ruth K alipoulizwa kuhusu suala la ujauzito aliweka wazi kuwa hana uhakika kama ni mjauzito.
Huku akiwashirikisha mashabiki katika kipindi cha Maswali na Majibu kwenye Instagram, Ruth ambaye anadaiwa kuwa katika uhusiano wa kimapenzi na Mulawah hata hivyo alidokeza kuwa kwa sasa ana hamu ya “vitu kali”.
Shabiki mmoja alimuuliza kama ana mimba, naye akajibu “Sijui kama iko lakini niko na hamu ya vitu kali.”
Ufafanuzi huu ulikuja baada ya wanamitandao kueneza tetesi kuwa muigizaji huyo mrembo huenda amembeba mtoto tumboni.
Tetesi kuwa Ruth ni mjamzito zilianza mwishoni mwa mwezi Julai kutokana na video yake na Mulamwah ambapo tumbo lake lilionekana kuchomoza. Maoni ya mashabiki yalionyesha kuwa walisisimuliwa na Ruth kuwa mjamzito.
Kwa muda mrefu, mchekeshaji Mulamwah na Ruth wamekuwa wakidaiwa kuwa wapenzi. Wawili hao hata hivyo mara nyingi wameeleza kuwa wao ni marafiki wakubwa tu na wamezoea kuitana ‘bestie’, kumaanisha ‘rafiki bora.’