Seneta wa Kakamega Boni Khalwale amefunguka sababu kuu yake yeye kutoweka wazi idadi kami ya watoto wake.
Katika mahojiano na gazeti la The Star, Khalwale mwenye umri wa miaka 63 alikiri kwamba ni kweli watoto anaowasherehekea kufuzu katika mitihani ya kitaifa karibia kila mwaka ni kweli ni wake lakini akakataa katakata kuweka wazi idadi kamili ya wanawe kwa jumla.
Khalwale alisema kuwa katika familia yake ana historia ya kuzaa mapacha kutoka ukoo wa nyanya yake.
“Ni kweli ni mimi ambaye hupakia hao watoto kwa jumbe za kuwahongera na pia ni kweli watoto ninaowapost ni wangu. Sababu ambayo mnaniona nikiwa huru kufanya vile kila wakati ni kwa sababu niko na historia ya mapacha. Nyanya yangu alikuwa pacha. Babangu alikuwa pacha. Kwa hiyo jeni za upacha ziko ndani yangu,” alisema.
Mwanasiasa huyo alikiri kwamba hata katika uzao wa familia yake, ana watoto mapacha akisema kuwa wake zake wa pili na wa tatu walimzalia mapacha mara tatu.
“Sasa hivi nina makundi mawili ya mapacha vyuo vikuu. Kwa jumla nina watoto 5 vyuoni sasa hivi,” Khalwale alisema.
Alidinda kusema idadi kamili ya wanawe akizua kwamba kwa mila na tamaduni za watu kutoka jamii ya Abaluhya, ni mwiko kuhesabu idadi ya watoto.
“Wakati nitaacha kuhesabu, hapo ndipo ninaweza kusema idadi ya wanangu. Lakini kwa Mluhya kamili wa damu kuhesabu watoto ni hakufai kukoma hadi pale utakapoanguka na kuzirai,” aliambia gazeti hilo.
Gazeti hilo lilisema kwamba Khalwale ni mpenzi mkubwa sana wa tamaduni za Waluhya akisema kwamba usomi wake wa kiwango cha juu haukumtoa hata kidogo katika tamaduni za jamii yake pendwa.
“Kiingereza changu kingi na masomo yangu hayakunitoa katika Uluhya ambako nilikulia, wakati ninarudi kwenye tamaduni za jamii yangu huwa nakuwa mtanashati wa kuvutia,” alisema.