Mchekeshaji Mulamwah amekoshwa na shabiki wake mmoja ambaye alifanya tukio kubwa ili kumuenzi mcheshi huyo.
Mulamwah kupitia Instastory yake alipakia picha ya kiwambo cha simu yake akionesha maongezi baina yake na shabiki huyo aliyemtafuta baada ya kuanzisha ujasiriamali.
Shabiki huyo alianza kwa kumtaarifu Mulamwah kwamba amekuwa akimfuatilia kwa muda mrefu na anatokea Kakamega.
Alisema kwamba baada ya kupata mabawa kidogo na kupaa kuja Nairobi, alijikita katika mtaa ulioko nje kabisa ya jiji, Rongai na kwamba amefungua biashara ya kuuza nyama na kuamua kuipa jina la Mulamwah.
“Habari yako Mulamwah, jina langu ni Benson, shabiki wako shupavu kutoka Kakamega lakini kwa sasa niko Ongata Rongai. Nikiwa kama shabiki wako namba moja, pamoja na mke wangu tumefungua biashara ya kuuza nyama na kuita jina lako. Tunatumai siku moja utafika huku kwa biashara yetu, Mungu akubariki sana,” Benson alimwandikia Mulamwah.
Mulamwah alishangazwa na kitendo hiki kisichoweza kulipiwa na kumuahidi shabiki huyo kwamba hivi karibuni atafanya ziara kwa biashara yake ili kuchoma nyama pamoja kama njia moja ya kuenzi ushabiki usio na kifani.
“Wow, ahsante sana, nimenyenyekea sana, lazima nitakuja huko tuchome nyama,” Mulamwah alimwambia Benson.
Hili linakuja siku chache baada ya msanii kutoka Tanzania Harmonize kuonesha furaha yake kwa shabiki aliyechora picha yake kubwa nyuma ya tuktuk yake.
Akipakia klipu hiyo, Harmonize aliahidi kumtunuku shilingi laki 5 za kitanzania shabiki yeyote ambaye atachora picha yake kwenye chombo chake cha usafiri, akiahidi pia atatoa kiasi sawa na hicho kwa yule atakayeweka picha yake na ya Hamisa – anayemuita rafiki wake wa kufa kuzikana.