Wikendi iliyopita ulikuwa ni wakati wa kihistoria na wa kukumbukwa milele katika maisha ya kimuziki ya msanii Harmonize baada ya kushinda tuzo 3 kwa mpigo katika hafla iliyoandaliwa nchini Marekani.
Harmonize alishinda tuzo 3 kwa kuwabwaga wasanii wakubwa wa Afrika katika tuzo za African Entertainment Awards.
Tuzo ya kwanza aliyoshinda kwa kura nyingi ni tuzo ya msanii bora wa mwaka barani Afrika, akashinda pia video bora ya mwaka kupitia ngoma yake ya Single Again na pia akatajwa kama mfalme wa muziki wa Afrika Mashariki na Bongo Fleva kwa jumla.
Katika tuzo hizo, Harmonize aliwaonyesha kivumbi wasanii kama vile Libianca kutoka Cameroon ambaye amekuwa akifanya vizuri, Asake, Burna Boy, Davido, Tiwa Savage, Yemi Alade, Rema wote kutoka Nigeria lakini pia Diamond Platnumz kutoka nyumbani Tanzania.
Baada ya kuchukua tuzo hizo kwa mpigo, msanii huyo kupitia Instagram yake alidokeza kwamba mwakani sherehe itakuwa kubwa Zaidi ambapo anatarajia kuzinyakua tuzo karibia zote.
Harmonize aliendeleza kuipigia upato albamu yake ambayo ataizindua siku kumi zijazo na kuweka kionjo cha ngoma yake ya ‘Personal Trainer’ kutoka kwa albamu hiyo.
“Hakikisha Unatembelea Bongo 💿 Novemba 24 ❤️ Nilifanya hii kuwa Maalum kwa Wasichana Wote Wakali kwenye GYM huko nje 🏋️♀️ 🏃♀️ huu ni mpango wako wa mazoezi Jumatatu hadi Jumapili Kutoka kwa Mkufunzi wako wa kibinafsi KONDEBOY 🏋️♂️ fuata Mpango huu #visitbongo💿 24/11/2023 Wanawake Fanyeni Changamoto hii kwenye Tiktok sasa !!!!! Waonyeshe Jinsi Unavyofanya 🏋️♂️ Niwaahidi Tu, Mwakani tunabeba Kila Tuzo Panapo Majaaliwa Inshaallah!!! tuliwasilisha Albamu bora zaidi 💿 tuonane Novemba 24,” Harmonize aliandika.