•Zari alikuwa akiwasherehekea wanaume wawili hao muhimu maishani mwake wakiadhimisha siku yao maalum, siku yao ya kuzaliwa.
•Shakib alifikisha umri wa miaka 32 Jumanne wakati Prince Nillan anasherehekea siku yake ya saba ya kuzaliwa leo, Desemba 6.
Usiku wa kuamkia Jumatano, mwanasosholaiti na mfanyabiashara maarufu wa Uganda, Zari Hassan aliandika ujumbe mzuri kwa mumewe Shakib Cham Lutaaya na mwanawe mdogo Riaz Nasibu Abdul almaarufu Prince Nillan.
Mama huyo wa watoto 5 alikuwa akiwasherehekea wanaume wawili hao muhimu maishani mwake wakiadhimisha siku yao maalum, siku yao ya kuzaliwa.
Katika ujumbe wake kwa wawili hao, mwanasosholaiti huyo mwenye umri wa miaka 43 alimwomba Mungu atimize matamanio yao yote ya moyo.
"Nisaidieni kuwatakia mume wangu na mwanangu siku njema ya kuzaliwa.. Mwenyezi afanye mapenzi yako yote yatimie," Zari Hassan aliandika kupitia ukurasa wake wa Instagram.
Aliambatanisha ujumbe wake na picha ya Shakib na Prince Nillan wakiwa wamesimama kando huku wakiwa wamevalia suti za kijivu zinazolingana. Wawili hao walionekana vizuri pamoja.
Shakib alifikisha umri wa miaka 32 Jumanne, Desemba 5 wakati Prince Nillan anasherehekea siku yake ya saba ya kuzaliwa leo hii, Desemba 6.
Prince Nillan ni mtoto wa Zari Hassan na aliyekuwa mpenzi wake, mwimbaji Diamond Platnumz. Kwa upande mwingine, mwanasosholaiti huyo alifunga ndoa rasmi na Shakib katika harusi ya kupendeza mapema mwaka huu. Pengo la umri kati ya mama huyo wa watoto watano na mumewe hata hivyo limekuwa suala kubwa miongoni mwa mashabiki wao tangu uhusiano wao ulipojulikana hadharani mapema mwaka jana.
Mwanasosholaiti huyo alirudiana na Shakib mapema mwaka jana baada ya kukatiza mahusiano na mfanyibiashara wa Uganda GK Choppa. Waliweka mahusiano yao siri hadi katikati mwa mwaka jana ambapo walifichua wanachumbiana.