Mwanamuziki mkongwe Suzanna Owiyo ametia neno katika mada inayoendelea kuvutia hisia kinzani katika mitandao ya kijamii kuhusu aina ya miziki ya msanii kutoka Kisii, Chris Embarambamba.
Kupitia ukurasa wake wa X, Owiyo alisema kwamba ameketi chini na kujaribu kuchanganua aina na kile Embarambamba anasema ni miziki ya Injili lakini akashindwa kuelewa.
Owiyo alisema kwamba kutokana na ukakasi mwingi uliozingira kile ambacho msanii huyo wa Kisii anaita ‘injili’ yeye ameamua kuuona kwa darubini tofauti kabisa.
Msanii huyo wa kibao maarufu ‘Kisumu 100’ alisema kwamba anachofanya Embarambamba kama si cuahwi basi kinaweza kutafsirika kama filamu chafu za watu wazima.
“Ninajaribu sana kufafanua Muziki wa Embarambamba. Nisaidie kufafanua aina yake! Injili? Hapana. Hata hivyo, Mambo 2 huja akilini; Kukimbia usiku na Ponografia. Je, hii inaweza kuwa dalili za matatizo ya kiakili?... Nipo radhi kukosolewa,” Owiyo alisema.
Embarambamba amekuwa kwenye tanuru la moto baada ya kuachia kibao ‘Tuko Uchi’ akionekana kucheza densi akiwa uchi, shukrani kwa kijitaulo chembamba kwenye kinena chake.
Siku mbili zilizopita, bodi inayosimamia ubora wa kazi za kisanaa nchini KFCB ilitoa barua ya kumtaka msanii huyo kuondoa video hiyo katika mitandao yote ya kijamii la sivyo achukuliwe hatua kali za kisheria.