Alikiba aongeza kuni kwenye ushindani na Diamond, azindua kituo cha redio na TV

Ali Kiba alizingua Crown FM na Crown TV wakati akiadhimisha miaka 20 kwenye tasnia ya burudani.

Muhtasari

•Alikiba alizindua Crown FM na Crown TV siku ya Jumamosi jioni wakati akisherehekea miaka ishirini katika tasnia ya burudani.

•Alikiba anaungana na kina Diamond  na Francis Majizzo kwenye orodha ya mastaa  wanaomiliki vyombo vya habari.

Image: INSTAGRAM// ALIKIBA

Staa wa Bongofleva Ali Saleh Kiba almaarufu Ali Kiba ndiye mmiliki mpya wa chombo cha habari katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Bosi huyo wa Kings Music Records alizindua vituo vyake vya Crown FM na Crown TV siku ya Jumamosi jioni wakati akisherehekea miaka ishirini katika tasnia ya burudani.

Huku akizungumzia sababu ya kuamua kuzindua vituo vyake vya habari, staa huyo wa bongo fleva alibainisha kuwa redio na tv zimekuwa nguzo kuu katika kujenga taaluma yake ya muziki.

“Media ni chombo chenye nguvu sana, Media ndio iliyonifanya kuwa Alikiba huyu wa leo,” Alikiba alisema wakati wa uzinduzi wa vituo vyake.

Aliongeza, “Ila pia mimi nilikuwa silali bila redio yangu ndogo niliyoletewa zawadi na baba yangu kupigwa muziki. Changamoto nilizopitia na kutatua kuleta suluhisho kwenye media ndivyo ndivyo vimenipa msukumo."

Mwimbaji huyo mkongwe alitangaza kuwa Crown Media haitakuwa na kituo cha redio na tv pekee, bali pia itakuwa na majukwaa ya kidijitali ili kusaidia kufikia mahali ambapo hakuna mipaka na pia huduma ya usimamizi wa hafla ambayo itasaidia kufika pale mashabiki walipo.

“Crown ipo kwa ajili ya wote ambao wanatafuta majibu ya maswali yao, wanaoutafuta ubora na utofauti pamoja na kasi na huduma,” alisema Kiba.

Miongoni mwa wageni maalum waliokuwepo wakati wa uzinduzi wa Crown Media ni rais wa zamani wa Tanzania Jakaya Kikwete, waziri wa Habari, Mawasialiano Na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye, pamoja na wengine.

Alikiba sasa anaungana na kina Diamond Platnumz na Francis Ciza Majizzo kwenye orodha ya mastaa wa bongo wanaomiliki vyombo vya habari.

Diamond anamiliki Wasafi Media (Wasafi TV, Wasafi Radio) huku Majizzo ambaye pia mcheza santuri akimiliki E-FM na TV-E.