Mwanamuziki Esther Akoth almaarufu Akothee alionekana kuwa mzazi mwenye fahari baada ya binti yake mdogo Fancy Makadia kuchumbiwa na mpenzi wake Fairouz Vivian Ligali Ali.
Makadia na mpenzi wake walipeleka uhusiano wao katika hatua nyingine wakati walipokuwa likizoni kusherehekea siku ya kuzaliwa ya mtoto huyo wa tatu wa Akothee.
Msichana huyo mwenye umri wa miaka 24 alionekana kujivunia sana kukubali ndoa na mpenzi wake na akabainisha amefurahishwa na ukurasa wao mpya.
"Nasema 'I do' kwa milele na rafiki yangu bora," Fancy Makadia aliandika chini ya video ya iliyomuonyesha mpenzi wake akimvisha pete kidoleni.
Pia alishiriki video nyingine iliyonyesha akijigamba na pete ambayo mpenzi wake aliweka kwenye kidole chake na katika sehemu ya maelezo, akamtambulisha Bw Fairouz kama mpenzi wake wa roho.
"Nimefurahi kuanza sura hii mpya na mwenzi wangu wa roho," aliandika.
Makumi ya wanamitandao ikiwa ni pamoja na mamake Akothee na dada zake Rue Baby na Vesha Okello walikusanyika chini ya chapisho kuonyesha upendo kwake na kumpongeza.
“Ish!” Akothee aliandika.
Rue Baby akasema, “Aaalllllaaaaa eiiii.”
Vesha Okello: Eeeeish yawa.
Dadake Akothee Cebbie Koks pia alionyesha upendo wake kwa mpwa huyo wake wa miaka 24 kwa hatua kubwa ya kimapenzi aliyopigwa.
Makadia alisherehekea siku yake ya kuzaliwa ya 24 mapema wiki hii na alielezea furaha yake kuhusu sura mpya aliyofungua.
"Ujana wa miaka 24 leo! ��� Asante kwa mwaka mwingine uliojaa ukuaji, vicheko, na matukio ya kupendeza. Hapa ni kukumbatia kila fursa, kufukuza ndoto, na kuunda kumbukumbu zisizosahaulika. Hongera kwa mwaka uliojaa uwezekano usio na mwisho!,” alisema mnamo siku yake ya kuzaliwa.
Binti huyo wa tatu wa Akothee ambaye amekuwa akiishi Ufaransa kwa miaka michache iliyopita amekuwa kwenye uhusiano wa kimapenzi na Bw Fayrouz kwa muda sasa na wapenzi hao wawili hawajaona haya kuonyesha mapenzi yao mazuri hadharani kupitia mitandao ya kijamii.