Bobrisky, Mwanamume wa Nigeria aliyebadili jinsia yake kupitia upasuaji na kuwa mwanamke amegonga vichwa vya habari baada ya kutunukiwa kama mrembo aliyetokea kwa muonekano wa kuvutia Zaidi wakati wa uzinduzi wa filamu jijini Lagos.
Kijana huyo aliyejizolea umaarufu kwa uvaaji wake wa mavazi ya kike alitokea katika uzinduzi wa filamu ya Ajanaku: Beast of the Worlds Jumapili na aliteuliwa kama mtu aliyevalia vizuri Zaidi kwa wanawake wote, licha ya kuwa mwanamume.
Bobrisky ambaye alizaliwa na kupewa jina la Okuneye Idris Olanrewaju na wazazi wake, tangu afanye msururu wa upasuaji kuboresha muonekano wake, amekuwa akijitambua kama mwanamke.
Kijana huyo amekiuka vikwazo vyote na kujitambua hadharani kama mtu mwenye jinsia mbili licha ya sheria za Nigeria kuharamisha mtu yeyote kujitambua kuwa na jinsia mbili au kuwa mwanachama wa jumuiya ya LGBTQ.
Mwishoni wa mwaka jana, Bobrisky alionyesha kwa mara ya kwanza mabadiliko ya mwili wake baada ya kufanyiwa upasuaji mwingine wa kuboresha makalio yake.
Katika picha zilizotikisa hewani mtandaoni, Bobrisky akiwa amevalia mavazi meusi, alionekana akiwa amekaa vizuri kwenye kitanda chake, akionyesha sura yake mpya.
Bobrisky alinukuu, "Nzuri na ya kustarehesha, huo ni mtindo wangu."