Kwa mara nyingine, bosi wa WCB Wasafi, Diamond Platnumz ameona fahari kwa msanii wake wa kike Zuchu kwa kufikisha views Zaidi ya milioni 30.
Wimbo wa Honey ambao Zuchu aliutoa miezi 8 iliyopita umefikisha hadi watazamaji milioni 30.
Kupitia instastory yake, Diamond alichapisha kipande cha video hiyo na kusema kwamba Zuchu mahali amefikia ameshindikana kitakwimu, kwani kila wakati ni yeye tu anauruga na kuweka rekodi mpya za takwimu kwenye utiririshaji wa miziki yake.
Aidha, safari hii Diamond hakumtambua kama mpenzi wake bali alimtaja kama binti.
“Huyu binti kashindikana kabisa, kama mtambo wa namba mzima anauendesha yeye,” Diamond aliandika.
Hii inakuja siku chache baada ya wimbo wa Sukari wa Zuchu kuweka rekodi nyingine ya kuwa wimbo wa kwanza wa msanii binafsi bila kushirikisha au kushirikishwa kwenye kolabo kufikisha watazamaji milioni 100.
Zuchu amekuwa katika lebo ya WCB Wasafi tangu mapema 2020 na amechia vibao vingi lakini wengi bado wanahisi uwezo wake katika utunzi haujaupika uwezo aliowekeza katika kutunga ‘Sukari’.