Nataka kukumbatia karibu zaidi leo!- Ujumbe maalum wa Kate Actress kwa mwanawe anapokuwa mtu mzima

Mtoto wa kwanza wa muigizaji Kate Actress, Leon Kamau, anaadhimisha hatua muhimu sana maishani mwake.

Muhtasari

•Mwanawe Kate Actress alitimiza umri wa miaka 18, hatua inayomruhusu kutambuliwa rasmi kama mtu mzima nchini Kenya.

•Kate aliambatanisha ujumbe wake na picha ya kumbukumbu yake na Leon, na sala maalum sana kwa mvulana wa miaka 18.

Image: INSTAGRAM// KATE ACTRESS, KAMAU

Mtoto wa kwanza wa muigizaji Catherine Kamau almaarufu Kate Actress, Leon Isaac Kamau, anaadhimisha hatua muhimu sana maishani mwake.

Hivi majuzi, mvulana huyo wa muigizaji huyo maarufu alitimiza umri wa miaka 18, hatua inayomruhusu kutambuliwa rasmi kama mtu mzima nchini Kenya.

Kate ametumia fursa hiyo kusherehekea mwanawe kwa ujumbe maalum, akielezea kujali kwake kwa mbegu ya tumbo lake haswa katika wakati ambapo maisha ya vijana wengi wa Kenya yanachukuliwa kuwa hatarini.

"Nina hisia sana leo 😔, Kheri ya siku ya kuzaliwa ya 18 mtoto wangu mkubwa . Pamoja na yote yanayoendelea kutuzunguka,😔 akina mama kupoteza watoto wao wa kiume wasio na hatia kwa ukatili wa polisi & dhulma zingine anazofanyiwa mtoto wa kiume mweusi katika jamii ya sasa, nataka nikusogezee karibu zaidi leo, kwa kumshukuru Mungu sana kwa kupata. wewe kwa Umri huu mkubwa. Tulifanya mtoto wangu. Kheri ya siku ya kuzaliwa roho yangu,” Kate Actress alimwandikia mwanawe kupitia akaunti yake ya Instagram.

Muigizaji huyo mashuhuri aliambatanisha ujumbe wake na picha ya kumbukumbu yake na Leon, na sala maalum sana kwa mvulana wa miaka 18.

Leon alizaliwa miaka mingi iliyopita wakati Kate alikuwa anaendeleza masomo yake ya chuo kikuu katika nchi jirani ya Uganda.

Katika mahojiano ya miaka michache iliyopita, muigizaji huyo mahiri alifichua kuwa alipachikwa ujauzito wa kifungua mimba hicho chake  miezi mitatu tu baada ya kujiunga na chuo kikuu cha Kampala.

Kate alikiri kuwa aliponda raha kweli kuanzia siku za kwanza alipojiunga na chuo kikuu na alishtuka sana wakati daktari alipomvunjia habari kuhusu ujauzito wake.

"Ilikuwa kama uhuru. Ningeweza kuenda nje. Tulikuwa  karibu na Kabaragala, hepi kila wakati.. tulidunda. Hata sikupumua, miezi mitatu nikabeba ujauzito. Sikuelewa jinsi ilikuwa mshtuko kwangu, ilikuja haraka. Hata daktari aliponiambia sikuamini. Nilikuwa msichana mdogo na mtu hangejua. Sikufahamu kuhusu kutumia mbinu za kuzuia ujauzito. Niliendea dawa za 'Morning after' baada ya wiki tatu " Cate alisimulia katika mahojiano na Churchill.

Muigizaji huyo alidai kuwa jamaa aliyempachika ujauzito alimsaidia siku za kwanza lakini baada ya kuona jinsi mambo yalivyoendelea kuwa mazito akamuacha.