logo

NOW ON AIR

Listen in Live

“Hakukuwa na kesi” DJ Fatxo aeleza kwa nini hakuna aliyeshtakiwa kuhusu kifo cha Jeff Mwathi

Msanii huyo wa nyimbo za Kikuyu alisisitiza kuwa hakuwepo nyumbani kwake wakati marehemu Jeff alipofariki.

image
na SAMUEL MAINA

Burudani04 July 2024 - 07:39

Muhtasari


  • •Alieleza kuwa upande wa mashtaka haukuona sababu ya kufungua kesi kwa kuwa hakuna mtu aliyehusika katika tukio hilo.
  • •Msanii huyo wa nyimbo za Kikuyu alisisitiza kuwa hakuwepo nyumbani kwake wakati marehemu Jeff alipofariki.

Mwimbaji maarufu wa Mugithi Lawrence Njuguna almaarufu DJ Fatxo amezungumza kuhusu kifo cha Jeff Mwathi, zaidi ya mwaka mmoja baada ya kuhusishwa na tukio hilo.

Akizungumza katika mahojiano kwenye Obinna TV, mwimbaji huyo mwenye umri wa miaka 28 alibainisha kuwa hakuna aliyeshtakiwa kuhusu kifo cha kutatanisha cha marehemu Jeff Mwathi.

Alieleza kuwa upande wa mashtaka haukuona sababu ya kufungua kesi kwa kuwa hakuna mtu aliyehusika katika tukio hilo, kama ilivyodaiwa na wengi.

“Hakukuwa na kesi. Kilichotokea ni kwamba, baada ya DCI kufanya uchunguzi, waliwasilisha faili lao kwa DPP kwa ajili ya kuchunguzwa zaidi. Ndipo DPP baadaye akagundua kuwa hakuna kesi. Kesi huwa inaundwa katika afisi ya DPP, kisha wanaipeleka kortini ili wajue kama kuna mtu anayepaswa kushtakiwa,” DJ Fatxo alisimulia.

Aliongeza zaidi, "Katika hali nzima, hakuna mtu aliyeshtakiwa kwa sababu hakuna mtu aliyefanya kile ambacho watu walikuwa wanasema. Nilikuja kugundua baadaye kuwa kinachotokea mtu anapojitoa uhai, faili halifungiwi katika kituo cha polisi. Inapelekwa mahakamani ili hakimu awasikilize ninyi nyote mnaofikishwa mahakamani kama mashahidi wa serikali.

Pamoja na DCI ambao ni mashahidi, mimi ambaye nilikuwa naye siku nzima, na mtu yeyote ambaye alitangamana naye au mtu yeyote ambaye aliona kitu cha aina hiyo. Ikifika pale, hakimu atasikiliza kila mtu na hatimaye ana mamlaka ya kufunga faili na kusema kuwa hajamkuta mtu yeyote mwenye hatia.”

Msanii huyo wa nyimbo za Kikuyu alisisitiza kuwa hakuwepo nyumbani kwake wakati marehemu Jeff alipofariki.  Alimuomboleza marehemu akisema kwamba alipoteza rafiki mzuri sana.

"Alikuwa rafiki mzuri sana. Nikienda nawe nyumbani kwangu baada ya kutoka nje usiku, ina maana kwamba nakujali. Watu walikuwa wakali sana na wepesi wa kunihukumu.

Hakuna mtu alikaa chini akaona mimi ndio naomboleza zaidi. Mimi binafsi nilipoteza rafiki lakini watu walikuja na kuanza maneno mengi. Mungu anajua kila kitu,” alisema.

Jeff alipoteza maisha mnamo Februari 22, 2023 baada ya kuanguka kutoka orofa ya 12 ya Redwood Apartments, mtaa wa Kasarani alikokuwa akiishi DJ Fatxo.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved