Mchekeshaji Eric Omondi ametoa maoni yake kuhusu mkutano wa Rais William Ruto na Gen Z kwenye jukwaa la X space.
Akizungumza wakati wa mahojiano Eric Omondi ambaye amekuwa mstari wa mbele kukosoa utawala wa Ruto, alisema kuwa kama vijana hawako tayari kufanya mazungumzo yoyote na rais.
Eric alibainisha kuwa kukataliwa kwa Mswada wa Fedha uliopendekezwa ni kura ya kutokuwa na imani na utawala wa Ruto.
Pia aliongezea kwamba Wabunge waliounga mkono Mswada huo wenye utata pamoja na Mkuu wa Nchi wanapaswa kujiuzulu.
“Hatutaki! Hatutajoin. Tumepangwa ya kutosha. Tunataka Ruto aende. Chochote wanasema hatukubali,” alisema.
“Suluhu ya shida ya Kenya ni ikiwa Rais Daktari Ruto, waziri wake, na wale waliovote Ndiyo watajiuzulu. Ni kura ya kutokuwa na imani.”
Eric Omondi alizidi kufichua kuwa Wakenya wamechanganyikiwa kwa muda mrefu kutokana na gharama ya juu ya maisha na kuongeza kuwa Mswada huo wenye utata ulikuwa kichochezi tu.
“Wakenya wamesema sio Mswada wa Fedha, Mswada wa Fedha tumetumia kuongea uchungu na matakwa yetu."
"Bili ya fedha ni trigger tu. Hatutaki, hatukubali, tutambandua na tutatumia sheria,” alisema
Msemaji wa Ikulu Hussein Mohamed mnamo Alhamisi, Julai 4, 2024, katika chapisho kwenye X alifichua kuwa Ruto atashirikiana na vijana kwenye X Space leo kuanzia 2pm -5pm.
Rais William Ruto anatazamiwa kuwa mwenyeji wa mazungumzo yake ya kwanza ya X-Space (zamani Twitter) na vijana wa Kenya mwendo wa saa nane mchana hadi saa kumi na moja jioni leo.
Kulingana na Ikulu, baraza la mawaziri limepangwa kujiunga na majadiliano ya mtandaoni ya saa tatu. 'X Spaces', ni kipengele kinachokuruhusu kuwa na mazungumzo ya moja kwa moja ya sauti kwenye jukwaa la mitandao ya kijamii.
Wakenya wamealikwa kujiunga na mjadala wa X Space kuanzia saa nane mchana hadi saa kumi na moja jioni