Diana Marua, Bahati wazungumzia athari ya Askofu Kiuna wakimuomboleza kihisia

Bahati na Diana wametoa taarifa wakizungumzia jinsi kifo cha marehemu Kiuna kimewagusa.

Muhtasari

•Katika taarifa yake, mwanavlogu Diana Marua aliomba faraja ya Mungu kwa watu walioathiriwa sana na tukio hilo la kusikitisha.

•Bahati alimuomboleza marehemu askofu Kiuna na kuchukua fursa hiyo kuwafariji walioguswa na kifo hicho hasa familia ya marehemu.

Image: INSTAGRAM// DIANA MARUA

Familia ya Bahati imeungana na Wakristo wengine wengi wa Kenya kuomboleza kifo cha mwanzilishi wa kanisa la Jubilee Christian Church, Askofu Allan Kiuna.

Bahati na mke wake Diana Marua wametoa taarifa kwenye kurasa zao za mitandaoya kijamii wakizungumzia jinsi kifo cha marehemu Kiuna kimewagusa.

Katika taarifa yake, mwanavlogu Diana Marua aliomba faraja ya Mungu kwa watu walioathiriwa sana na tukio hilo la kusikitisha.

"Mungu wangu!!!! Niniii! Mungu Mpendwa, akufariji Mama, watoto wake, familia na Kanisa 😭😭😭😭,” Diana aliandika kwenye Instagram.

Aliambatanisha taarifa yake na picha kadhaa za kumbukumbu zake nzuri akiwa na marehemu Kiuna.

Aliendelea kumpongeza marehemu kwa athari aliyokuwa nayo katika maisha yake na kuomboleza kifo chake.

“Asante Askofu kwa Mwongozo wako. Umetufundisha vizuri. Cheza na Malaika Bwana! Leo ni siku ya Giza kwa wengi wetu tuliokufahamu kwa kiwango cha kibinafsi 😭 Moyoni mwangu, nitakukumbuka daima. Ni vigumu kusema hivi, Nenda vizuri Askofu Kiuna 🕯️😭,” aliongeza.

Kwa upande wake, mwimbaji Bahati naye alimuomboleza marehemu askofu Kiuna na kuchukua fursa hiyo kuwafariji walioguswa na kifo hicho hasa familia ya marehemu.

 “Pumzika kwa amani mtu wa Mungu💔 💔 💔 Mungu Amtie Nguvu Mama Kathy, Familia na Usharika mzima wa Kanisa la JCC,” Bahati aliandika.

Siku ya Jumanne, Kanisa la Jubilee Christian Church (JCC) liliomboleza kifo cha mwanzilishi na mchungaji kiongozi wake, Askofu Allan Kiuna, aliyeaga dunia baada ya kuugua saratani ya Multiple Myeloma.

Askofu Kiuna alikuwa akipokea matibabu nje ya nchi na hapo awali alitangaza uponyaji wake kutoka kwa saratani mnamo 2023.

Safari yake kupitia ugonjwa ilianza Desemba 2022 aliposafiri hadi Marekani kwa ajili ya matibabu.

Licha ya safari hiyo ngumu, alirudi kwenye kutaniko lake ili kujitangaza kuwa hana saratani, na kutoa shukrani nyingi.

"Kwa mwaka mmoja niliokuwa Marekani, matibabu yangu yaligharimu dola milioni 3, na sikutoa sarafu moja mfukoni mwangu kwa sababu Mungu wa mbinguni alinipa. Sikumpigia simu mtu yeyote,” alisema, akipokea shangwe kutoka kwa kutaniko.

Hapo awali Askofu Kiuna alikiri vita vyake dhidi ya saratani mwaka wa 2019 na akatangaza kupona akiwa amesimama kwenye madhabahu ya kanisa hilo.

Ameacha mke wake, Cathy Kiuna, na watoto wao watatu: Vanessa, Jeremy, na Stephanie.