Mchekeshaji aliyegeuka na kuwa mwanaharakati Eric Omondi ameibua madai kwamba alikuwa na taarifa za kuvunjwa kwa baraza la mawaziri na rais Ruto mwendo wa Jumatano usiku.
Akizungumza kwenye runinga ya Citizen asubuhi ya Ijumaa, Omondi alisema kwamba hatomtaja mtu ambaye anadai alimdokezea taarifa hizo, lakini akasema kuwa alikuwa na uhakika wa kuvunjwa kwa baraza la mawaziri majira ya saa tano usiku.
Rais Ruto alitoa tangazo la kuvunjwa kwa baraza la mawaziri mwendo wa saa tisa alasiri siku moja baadae – Alhamis.
Omondi alikuwa anajibu tetesi kwamba alikuwa ametishia kufanya maandamano hadi katika ikulu ya rais siku ya Alhamis asubuhi lakini baada ya kupata taarifa hizo usiku wa Jumatano, alilazimika kurudisha kwenye kikapu tishio hilo.
“Kumbuka Jumanne nilikuwa nimemuomba rais Ruto kulivunja baraza lake la mawaziri kufikia Alhamisi…mimi nilijua kufikia Jumatano usiku wakati Moses K uria alikuwa anaondoka katika studio hizi, kwamba Ruto amefuta mawaziri wote, kufikia saa tano usiku. Siwezi kusema ni nani aliniambia lakini nilijua kwamba wote vibarua vyao vimeota nyasi,” Eric Omondi alisema.
Hata hivyo, alisema kwamba bado rais Ruto ako na kibarua kigumu mbele yake kwani kila mtu anasubiri kuona mawaziri wapya atakaowateua.
Omondi kwa upande wake alisema kwamba hii ndio nafasi ya Ruto kuonyesha watu waliompigia kura kwamba anajali maslahi yao kwa kuteua watu wa boda boda na mama mboga kwenye baraza lake la mawaziri.
Rais Ruto alitangaza kuvunja baraza lake la mawaziri na kuwatuma nyumbani wote akiwemo mwanasheria mkuu wa serikali lakini waziri mwenye mamlaka makuu Musalia Mudavadi na naibu rais Rigathi Gachagua wakaponea shoka hilo.