Queen Rosie, binti aliyegonga vichwa vya habari siku kadhaa zilizopita kwa kuimba wimbo wa kusifia msanii Bunny Asila kwa matendo yake mema kwa watu wenye ugumu wa maisha amethibitisha kutambuliwa na msanii huyo mwenye makao yake nchini Ufini.
Binti huyo katika video ambayo imeonekana na Radio Jambo, alifichua kwamba baada ya kuimba wimbo wa kumuomba Bunny Asila msaada wa kimasomo na pia kumshika mkono ili talanta yake ya uimbaji ipate kunawiri, hatimaye video hiyo ilimfikia Asila na kumgusa.
Rosie akiwa na mama yake, alithibitisha kwamba Asila alifika nyumbani kwao na kumpa msaada wa karo ya shule, jambo ambalo walishukuru pakubwa yeye na mama yake.
Kando na kumlipia karo ya shule, binti huyo pia alifichua kwamba Bunny Asila aliwaahidi kuwafadhili ziara ya kufika jijini Nairobi.
“Leo niko hapa na mama yangu, tumefurahia sana venye Bunny Asila amekuja huku akaingia hadi kwa nyumba, akanilipia karo ya shule na kusema kwamba leo tunaenda Nairobi, nimefurahi sana,” binti huyo mdogo alisema.
“Niko na furaha sana Bunny Asila umenipunguzia mzigo na Mungu akubariki sana Asila mtoto wangu,” mama mtu aliongeza.
Nyota ya jaha ilianza kumtafuta msichana huyo baada ya video ya wimbo wake akiomba msaada kutoka kwa Asila kuenezwa mitandaoni.
“Niaje Bunny Asila, nataka kusikika, naomba unisapoti nijenge langu jina…. Naomba daily kama Paulo na Sila, nikuwe mtrue kama Bunny Asila, msanii mpole tena hana hasira, kijana mngori tena hana ukabila… kwa hao watano uniokote niende majuu pia mimi nionwe,” sehemu ya mistari katika wimbo wa binti huyo iliimba.
Hata hivyo, ni vizuri kukumbuka kwamba hii si mara ya kwanza kwa Asila, msanii kutoka Busia aliyekulia Nakuru kabla ya kupaa kwenda Ufini, kunyoosha mkono wake wa fadhila kwa watu wenye ugumu wa maisha.
Mwezi mmoja uliopita, msanii huyo aliahidi kutoa msaada wa maji na vinywaji vya burudani kwa waandamani wa Gen Z mijini Nakuru na Nairobi wakati wa shinikizo za kutaka serikali kuwajibikia matumizi yake ya ushuru.