Tony Sherman, kijana aliyegonga vichwa vya habari wiki moja iliyopita baada ya kudai kupata mpenzi katika maandamano ya Gen Z amezungumza.
Katika mahojiano na blogu ya SPM Buzz, Sherman alielezea jinsi alipata ujasiri wa kumtongoza mwanamke ambaye hawakuwa wamekutana na mara yao ya kwanza kukutana ni kwenye maandamano hayo ya kupinga serikali.
“Ilikuwa katika maandamano ya kwanza kabisa kufanyika, ilikuwa Jumanne. Mimi nilikuwa nimetoka tu nyumbani nikijua naenda maandamano, katika harakati hizo mambo mengi yalifanyika. Halafu ghafla nilimuona Kendi, akiwa amejitenga na waandamanaji wengine,” Sherman alisema.
Kutoka hapo alisema kwamba alimuona kuwa mtu tofauti na wengine na akaamua kumkaribia ili kupata usemi wake.
“Niliamua kumkaribia kwa sababu niliona kidogo amejitenga hivyo tu kwa mbwembwe. Niliona hata kama ako mmoja wetu lakini alikuwa mpweke. Baadae tulipoenda kuketi ndio alinielezea na kunitaarifu kwamba hakuwa amekuja kushiriki maandamano bali alikuja shughuli zake lakini mambo hayakuenda kulingana na matarajio yake.”
Kijana huyo alisema kwamba ndoa yake itafanyika hivi karibuni na angependa sherehe kufanyika katikati mwa jiji la Nairobi ambapo walikutania wakati wa maandamano.
“Kwa sababu tulikutana jijini, ningependa harusi yangu ifanyike jijini. Inawezekana, na itafanyika pale mbele ya Archives. Na huu si mzaha. Niliamua hivyo kwa sababu tunataka kuonyesha watu wenye hawako mtandaoni na wanafanya shughuli zao huko jijini na wanajua kwamba tulipatania kule ndio kila mtu aone tu,” alisema.
Wiki moja iliyopita, Sherman kupitia ukurasa wake wa Instagram alichapisha ujumbe akiwa na picha ambayo amempakata mpenzi wake na kuitangazia dunia kwamba anampenda sana.
“Ikiwa "haraka sana" alikuwa mtu. Wiki 3 tu baada ya kukutana na mechi yangu kamili ya maandamano, niliamua kumpendekeza. Nakumbuka wote wawili tulikuwa na bango lililoinuliwa sana wakati wakiimba "Ruto lazima Aende" katikati ya wimbo tulipaswa kujuana zaidi, na hapa tumefikia sasa! kuchumbiwa kwa furaha. Nakupenda Kendi,” Alisema.