Msanii bosi wa lebo ya muziki ya Konde Music Worldwide, Rajab Kahali maarufu kama Harmonize kwa mara ya kwanza amefichua ndoto ya kile anachowazia kukifanya wakati atakapostaafu kutoka ulingo wa Sanaa.
Katika mahojiano, msanii huyo alieleza kwamba anafahamu fika hatodumu kwenye muziki maisha yake yote na tayari ameshatambua kile atakachoridhika kukifanya baada ya viwango vyake vya muziki kushuka.
Harmonize ambaye miezi michache iliyopita alisherehekea kufikisha umri wa miaka 30 alifichua kwamba ana ndoto ya kuwa daktari kwa ajili ya kusaidia maisha ya binadamu, na angependelea kusomea udaktari baada ya kustaafu muziki katika umri wa miaka 45 hadi 50 hivi.
“Nishawahi kufikia kwamba mbeleni kazi zangu za Kimuziki zikipungua umri nikishakuwa labda umri umeshaenda labda Mungu akitufikisha kwenye miaka 45-50 nitafikiria kusomea udaktari. Angalau kwa mwaka basi niwe nafanya kazi kwa hospitali hata kwa wiki tu ili kuokoa maisha ya watu, kuwasaidia watu,” Harmonize alisema.
Msanii huyo alisema kwamba kando na kwamba lengo lake ni kutaka ktoa msaada wa kibinadamu zaidi kwa kutibu wagonjwa, lakini pia angependa kuona furaha ikiota katika nyuso za watu kutokana na taaluma hiyo ambayo anafikiria kuisomea.
Itakumbukwa hivi majuzi wakati anazungumzia maboresho yake katika uzungumzaji wa lugha ya Kiingereza, msanii huyo alifichua kwamba elimu yake ni ya darasa la 7 tu na kwamba hakuwahi kuenda shule yoyote au kutafuta huduma za mwalimu kumfunza Kiingereza bali ni bidii yake tu.
Awali, aliwahi nukuliwa akisema na hata kuimba kwenye moja ya tungo zake kwamba ndoto zake tangu utotoni zilikuwa kuwa mwanasoka.
Sasa inasubiriwa kuonwa ni vipi atafanikisha ndoto yake ya kuwa daktari, ikizingatiwa kwamba hakuweza kuejiendeleza kimasomo zaidi ya darasa la saba kama alivyokiri mwenyewe.