Ruth K, mkewe mchekeshaji Mulamwah ametoa taarifa njema kwa mashabiki wake Kamba amepata ajira ya ualimu.
Kupitia chaneli yake ya YouTube, Ruth K alifichua taarifa hizo kwa hisia akisema kwamba licha ya kuwa na furaha kupata ajira kama mwalimu, pia ana wasiwasi kuhusu muda wake mitandaoni, akisema huenda akaadimika pakubwa.
Mrembo huyo alikumbuka safari ya maisha yake na mumewe Mulamwah akisema kwamba tangu mwaka jana mambo yamekuwa yakitengemaa kwa upande wao.
“Mwaka jana Mungu alinibariki sana, nili’graduate, huo ndio mwaka tuliunda Kalamz, tukafanya sherehe nyumbani na mwaka huu tukianza Mungu akatubariki na mtoto, gari la kifahari, tumehama kutoka ghetto, yani hivi vitu ni Baraka za Mungu tu,” alisema.
“Mimi najua ni kuamini Mungu, bidii kidogo, Mungu mbele na mambo inajipa. Kitu chochote kinawezekana. Baraka nyingine ni kwamba niko na habari njema na habari mbaya. Tuanzeni na habari njema ni kwamba nimepata kazi kama mwalimu. Team teaching walimu hoyeee! University of Eldoret members hoyee! Hiyo ni Baraka kwangu wangu wangu.”
“Na habari mbaya ni kwamba mitandaoni mtaniona kweli? Mtakuwa mnaniona kidogo kidogo nitajaribu tu kwa kuchungulia. Nina furaha sana, wakati wa Mungu ukifika umefika tu hakuna mtu anaweza zuia,” aliongeza.
Pia alisherehekea kufikisha wafuasi zaidi ya laki moja kwenye chaneli hiyo chini ya miezi miwili.
Baraka hizi zinajiri siku chache tu baada ya kusherehekea siku yake ya kuzaliwa na pia kufichua sura ya mwanao kwa mashabiki wao katika mitandao ya kijamii.