Pozee, kama anavyojiita msanii wa humu nchini Willy Paul anazidi kula bata na kuruka kwa pipa katika mataifa ya Ulaya na Uarabuni.
Msanii huyo ambaye mwezi mmoja uliopita alitangaza kuhamisha makazi yake na shughuli zote za muziki kutoka Kenya kwenda Ujerumani sasa anajitambua kama ‘Mr International’ kwa maana kwamba yeye ni mtu anayejihusisha na shughuli za kimataifa.
Wikendi hii, anatarajiwa kutumbuiza nchini Saudi Arabia na ametangaza kutua jijini Riyadh tayari kwa shoo yake hiyo.
“Saud Arabia Mr International Amewasili Sasa…Jitayarishe Kwa Muda Mzuri Siku ya Jumamosi ya tarehe 27. Riyadh, Saudi Arabia,” Pozee aisema.
Msanii huyo tangu kuachia albamu yake ya Beyond Gifted, amekuwa akipokea sifa kubwa na albamu yake ikivutia watu wengi licha ya kutomshirikisha msanii hata mmoja wa humu nchini.
Itakumbukwa mwezi mmoja uliopita, Pozee alitumbuiza nchini Uholanzi mbele ya umati uliosisimka na kufurika na baadae kutangaza kuhamia nchi jirani ya Ujerumani.
Wiki chache zilizopita, alisema kwamba wimbo wake wa Lululala ulikuwa ukifanya vizuri nje ya Afrika Mashariki, akijitaja kama msanii pekee wa Kenya mwenye uwezo huo wa kipekee kuvuma nje ya ukanda huo.