logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Simu maalum kutoka kwa Leonard Mbotela yamfanya Gidi kujawa na machozi machoni

Mtangazaji huyo alifichua kuwa Bw Mambo Mbotela ni shabiki wake mkubwa na humpigia simu karibu kila siku.

image
na SAMUEL MAINA

Burudani27 July 2024 - 09:55

Muhtasari


  • •Mtangazaji huyo mahiri alifichua kuwa Bw Mambo Mbotela ni shabiki wake mkubwa na humpigia simu karibu kila siku.
  • •"Ni mtangazaji wa redio mcheshi sana wa wakati wetu.Mungu aendelee kukubariki Mbotela. Wewe ni msukumo kwa kizazi chetu,” alisema.
Leonard Mambo Mbotela na Gidi wa Radio Jambo.

Mtangazaji wa kipindi cha Gidi na Ghost asubuhi kwenye Radio Jambo, Gidi Ogidi amefichua uhusiano wake wa karibu sana na nguli wa redio, Leonard Mambo Mbotela.

Katika taarifa yake siku ya Ijumaa, mtangazaji huyo mahiri alifichua kuwa Bw Mbotela ni shabiki wake mkubwa na humpigia simu karibu kila siku.

Gidi alizungumza kuhusu mazungumzo maalum ya simu ambayo alikuwa nayo na nguli huyo wa redio siku ya Ijumaa ambayo yalimjaza hisia.

"Mtangazaji gwiji wa redio Leonard Mambo Mbotela huwa ananipigia simu karibu kila siku, ili kunijulia hali na kunikumbusha kuwa huwa anasikiliza kipindi changu, yeye ni shabiki mkubwa," Gidi alisema kupitia akaunti yake ya Facebook siku ya  Ijumaa.

Aliendelea, “Simu ya leo imeleta machozi kwenye macho yangu,  yeye ni mzee na anatulia ndani ya nyumba. Hawezi tena kubarizi nje kama hapo awali kwa sababu umri mkubwa umemshika, lakini bado anafahamu sana kinachoendelea."

Gidi alisifu uhalisia na ucheshi wa Bw. Mbotela, na akamwomba Mungu aendelee kumbariki.

"Yeye ni mtangazaji wa redio mcheshi sana wa wakati wetu.  Mungu aendelee kukubariki Mbotela. Wewe ni msukumo kwa kizazi chetu,” alisema.

Hii si mara ya kwanza kwa mtangazaji Gidi kudokeza kuhusu uhusiano wake wa karibu na nguli wa redio, Leonard Mambo Mbotela.

Takriban miezi miwili iliyopita, Gidi na mtangazaji mwenzake Ghost Mulee walimsherehekea mtangazaji mkongwe ambaye alikuwa anasherehekea siku yake ya kuzaliwa.

Watangazaji hao wawili walimsherehekea Mbotela kama mtu wanayemwiga na kupongeza kazi  yake nzuri na maisha marefu ambayo amekuwa nayo.

“Leo ni siku ya kuzaliwa kwa gwiji wa utangazaji hapa nchini Kenya Leonard Mambo Mbotela ambaye anatusikiza sasa hivi. Huyu ni jamaa ambaye ameishi miaka 84,” Gidi alisema moja kwa moja hewani wakati wa kipindi chao cha asubuhi.

Kwa upande wake, Jacob Mulee alibainisha kuwa mtangazaji huyo mkongwe ni rafiki yao mkubwa na pia ni shabiki wa kipindi chao cha asubuhi kwenye Radio Jambo.

Kocha huyo wa zamani wa Harambee Stars slibainisha kuwa wamejifunza mengi kutoka kwa Bw Mbotela ambayo yamewasaidia kuwa watangazaji wa kusherehekewa pia.

“Hiyo ni baraka ya Mwenyezi Mungu Gidi. Na ni rafiki yetu kwa dhati, nisikilizaji pia wa Radio Jambo. Na sisi utangazaji wetu tumetoa kwa Gidi kama yeye. Kwa hiyo, Kheri ya siku ya kuzaliwa Maje Maje,” Ghost alisema.

Watangazaji hao wawili waliendelea kufanya mzaha kuhusu kipindi maarufu cha  ‘Je, huu ni Ungwana’ ambacho Bw Mbotela alijulikana nacho kabla ya kumuimbia wimbo wa ‘Happy Birthday’. Pia walimtakia maisha marefu na yenye afya mtangazaji huyo mkongwe.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved