Staa wa Dancehall kutoka Jamaica, Adidja Palmer almaarufu Vybz Kartel ameachiliwa kutoka gerezani baada ya kufungwa kwa karibu miaka 13 kwa kupatikana na hatia ya mauaji.
Jumatano alasiri, mahakama ya rufaa ya Jamaica ilitoa uamuzi dhidi ya kusikilizwa tena kwa kesi hiyo, ikitaja sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na utovu wa nidhamu wa baraza la waamuzi na kuzorota kwa afya ya msanii huyo.
Mahakama ya Rufaa, ikiongozwa na Jaji Marva McDonald-Bishop, iliamua kwa kauli moja kuwaachilia Vybz Kartel na washtakiwa wenzake, Shawn ‘Shawn Storm’ Campbell, Andre St John, na Kahira Jones.
"Kwa kuzingatia masuala yote ambayo mahakama imezingatia, tunahitimisha kwamba maslahi ya haki hayahitaji kesi mpya kuamriwa kwa wakata rufaa," alisema Jaji Marva McDonald-Bishop.
"Kwa hiyo tunatoa amri ifuatayo: hukumu na uamuzi wa kuachiliwa huingizwa kuhusiana na wakata rufaa," aliongeza.
Zaidi ya miaka kumi iliyopita, mnamo Machi 2014, mwimbaji huyo wa dancehall alihukumiwa kifungo cha maisha kwa mauaji ya Clive 'Lizard' Williams.
Machi mwaka huu, hukumu hizo zilibatilishwa kutokana na utovu wa nidhamu wa baraza la waamuzi wa mahakama.
Msanii huyo msanii mpendwa huyo wa Dancehall alitoka nje ya Kituo cha Kurekebisha Watu Wazima cha Tower Street katikati mwa jiji la Kingston Jumatano alasiri, Julai 31. Hatua hiyo imezua msisimko mkubwa kutoka kwa mashabiki wa mwanamuziki huyo.
Itapendeza kuona atakapotumbuiza kwa mara ya kwanza, au atakapoanza kushirikiana na wasanii wengine wakubwa ambao wamekuwa wakipigania uhuru wake miaka hii yote.