Hamisa ajivunia mwanawe akitimiza miaka 7 huku Diamond akisafiri Afrika Kusini kum'surprise Tiffah

Hamisa alimtambua mwanawe kuwa ni mtoto mzuri, mwenye busara na baraka katika maisha yake.

Muhtasari

•Mpenzi huyo wa zamani wa Diamond amesherehekea athari nzuri ambayo mvulana huyo mdogo amekuwa nayo katika maisha yake.

•“Mwana wa bahari. Nuru ya macho yangu na furaha kwa roho yangu. Moyo wa mama ake @dylandeetz,” alisema.

Image: INSTAGRAM// HAMISA MOBETTO

Siku ya Jumapili, Agosti 11, mwanamitindo na msanii maarufu wa Tanzania Hamisa Mobetto alisherehekea siku ya kuzaliwa ya mtoto wake wa pili.

Dylan Mobetto aliadhimisha siku yake ya saba ya kuzaliwa hivi majuzi na mpenzi huyo wa zamani wa Diamond Platnumz amesherehekea athari nzuri ambayo mvulana huyo mdogo amekuwa nayo katika maisha yake.

Akizungumzia hilo, Hamisa Mobetto alimtambua mwanawe kuwa ni mtoto mzuri, mwenye busara na baraka katika maisha yake.

“Miaka 7 ya kuwa mama yako @dylandeetz. Namshukuru Mungu kwa ajili yako kila siku. Ahsante kwa kuwa mtoto mzuri na mwenye hekima. Wewe ni baraka na Faraja kubwa kwangu,” Hamisa Mobetto aliandika kupitia Instagram.

Aliambatanisha ujumbe wake na picha nzuri zake na mwanawe wakiburudika ufukweni.

“Mwana wa bahari. Nuru ya macho yangu na furaha kwa roho yangu. Moyo wa mama ake @dylandeetz,” alisema kwenye chapisho lingine.

Haya yanajiri miezi michache baada ya mwanamitindo huyo kufuta jina la Diamond kwenye jina la mwanawe. Hapo awali, mvulana huyo wa miaka saba alitambulika kama Dylan Abdul Naseeb kwenye mitandao ya jamii, lakini jina hilo limebadilishwa na sasa anatambulika kama Dylan Mobetto.

Licha ya mwanamitindo huyo wa Tanzania kumsherehekea mwanawe kwa ujumbe mzuri, mwanamuziki Diamond Platnumz ambaye wengi wanaamini kuwa ndiye baba wa mvulana huyo mdogo alikuwa bado hajamwandikia ujumbe wowote kufikia wakati wa kuchapishwa kwa makala haya.

Hili si la kushangaza sana kwani staa huyo wa bongo pia hakumsherehekea Dylan mnamo siku yake ya kuzaliwa miaka ya hivi majuzi.

Swali la ni nani baba halisi wa mtoto wa pili wa mwanamitindo Hamisa Mobetto limebaki kuwa kitendawili tu huku Diamond mara nyingi akionyesha dalili za wazi kuwa hamkubali au kumtambua mvulana huyo kuwa mwanawe.

Mwaka jana, rapa wa bongo Bill Nass alijitenga mbali na madai yanayomhusisha na mvulana huyo wa miaka sita.

Kwa muda mrefu, watu wamekuwa wakihusisha mtoto wa pili wa mwanamitindo huyo na Bill Nass na hata kuibua madai kuwa wanafanana sana. Bill Nass hata hivyo amedokeza kuwa tetesi za yeye kuwa baba wa mtoto huyo ni propaganda tu na kusema kuwa tayari Hamisa alikuwa na watoto wake wawili wakati walipofahamiana.

“Ni propaganda za watu. Sijui nia au dhumuni ya hiyo habari ilianzia wapi lakini mimi mtoto hanihusu kwa namna moja au nyingine. Wakati ambao tulifahamiana, tayari alikuwa na watoto wake wawili. Kwa mara ya kwanza namuona alikuwa na watoto. Kutokea hapo sijawahi kuwa na issue yoyote,” alisema kwenye mahojiano na Wasafi Media.