•Petro anamtuhumu kaka yake pacha, Paulo kwa kuharibu urithi wa bendi ambayo wote wawili waliijenga pamoja.
•Peter alielezea kusikitishwa kwake na hali ya sasa na athari ambayo P- Square imekuwa nayo kwa mashabiki wao
Wakiwa mapacha walioimba pamoja P-Square, walitawala muziki wa Afrobeat nchini Nigeria kwa miaka mingi na walikuwa moja ya vikundi vya kwanza kueneza muzikii huo katika sehemu nyingine za bara. Kuvunjika kwa kundi hilo kati ya pacha Peter na Paul Okoye waliofahamika maarufu P-Square ni jambo linalokaribia kukamilika.
Malumbano ya pacha hao wa Nigeria ambayo yamechochewa na migogoro ya ndani, kwa sasa hayaonyeshi dalili ya kumalizika wakati wowote hivi karibuni.
Barua ya wazi iliyowekwa kwenye mitandao ya kijamii ya mmoja wa mapacha hao kufuatia madai ya makosa ya kifedha yanayomhusisha mmoja wa pacha hao, imeonyesha kuongezeka kwa uhasama baina yao.
Katika chapisho kwenye Instagram na Facebook Jumatatu, Agosti 12, 2024, Peter "Mr. P" Okoye alielezea kusikitishwa kwake na wasiwasi wake juu ya msururu wa taarifa za umma za hivi karibuni za kaka yake, Paul "Rudeboy" Okoye, ambazo alisema zimepotosha ukweli kuhusu kazi yao kwa pamoja na michango yake ya kibinafsi kwa kundi hilo.
Petro anamtuhumu kaka yake pacha, Paulo kwa kuharibu urithi wa bendi ambayo wote wawili waliijenga pamoja.
"Kwa kaka yangu mpendwa Paul Okoye aka Rudeboy, kama ambavyo nimekua nikikuambia mara nyingi, siko katika ushindani na wewe au mtu mwingine yeyote.
Hata hivyo, kukuona unaposhiriki mahojiano mengi ukionyesha kudharau juhudi zangu katika kundi ambalo sisi wote tumeliunda na kulijenga pamoja ina maana kubwa.
Katika mahojiano yako ya hivi karibuni, unadai kuwa umeandika na kuimba 99% ya nyimbo za P Square na ulinidharau kwa kusema kwamba wimbo wetu na TI "EjeaJo" ambao niliandika haukufanikiwa.
Haukishia hapo ukaamua na kutumia maoni ya YouTube kunidhalilisha tena," aliandika katika ujumbe mrefu kwenye mitandao ya kijamii.
Peter alionyesha kusikitishwa na matendo ya ndugu yake, ambaye pia alimshutumu kwa kushirikiana na kaka yao mkubwa, Jude, ambaye alisema alikuwa anajaribu "kumkandamiza".
Alikanusha madai ya Paul kwamba alikuwa mtunzi mkuu na mwimbaji wa P-Square, akisisitiza kuwa mafanikio yao yalikuwa matokeo ya juhudi zao za pamoja.
Peter aliorodhesha nyimbo kadhaa za bendi hiyo, akishangaa ikiwa pia zilichukuliwa kuwa kama nyimba ambazo hazikufanikiwa. "Hujawahi kukiri nyimbo nyingine kama 'Get-Squared', 'Bizzy Body', 'Personally', 'Roll It', 'Temptation', 'Alingo', 'More than a Friend', 'Shekini', 'Say Your Love', 'Gimme Dat', 'Senorita', 'Igbedu' na nyingine chache. Je, nyimbo hizi pia hazikufanikiwa?"
Pia alilalamikia majaribio ya Paulo ya mara kwa mara ya kuidharau michango yake, akimshutumu kwa kuigeuza P-Square, ambayo ilikuwa kikundi cha muziki kilichopewa tuzo na kilichopata tuzo zaidi barani Afrika, kuwa "Kichekesho".
"Ni lazima ieleweke kwamba mashabiki hawakupenda P-Square kwa sababu ya nani aliimba au kucheza zaidi. Kilichotufanya tufanikiwe ni ubora wetu hali yetu iliotokana na juhudi zetu za pamoja – sisi wawili! P-Square ilikuwa ya nguvu, na mashabiki waliipenda P-Square kwa sababu ya upekee wetu na umoja, "aliongeza.
Pia alimkosoa Paul kwa kujilinganisha na Jude, akisema kuwa mienendo ya familia ilikuwa na jukumu kubwa katika matatizo ya bendi. "Ulimvunjia heshima mke wangu, familia yangu, kipaji changu, mawazo yangu na hata kuchukua upande wa Jude wakati alipokuwa anajaribu kunikandamiza."
Katika kukamilisha ujumbe wake, Peter alielezea kusikitishwa kwake na hali ya sasa na athari ambayo P- Square imekuwa nayo kwa mashabiki wao. "Sasa nahisi kama umechukua mambo hata zaidi kwa kujaribu kuwageuza mashabiki dhidi yangu kwa kuwafanya wafikiri nina wivu kwako. Umefanya kila kitu unachoweza kuwafanya mashabiki wanichukie, lakini unajua nini? Hawatanichukia kamwe; badala yake, watatuchukia sisi sote kwa sababu tuliwavunja moyo na kuwaangusha."
Makaka hao wa P-Square, ambao walitengana kwa mara ya kwanza mnamo 2017 kwa sababu ya kutoelewana kulikomhusisha kaka yao mkubwa, Jude Okoye, waliungana tena mnamo 2021, jambo lililowafurahisha mashabiki wao.
Ingawa chanzo halisi cha kusambaratika kwao hakijawahi kuwekwa hadharani, jumbe mbalimbali za mitandao ya kijamii walizozisambaza tangu kutengana kwao zimedokeza kuwa ugomvi huo uliwahusisha wake zao na kaka yao mkubwa, ambaye pia alikuwa meneja wao.
Baada ya kutengena kwao, wote walianza kazi za muziki kila mmoja peke yake chini ya majina Mr. P (Peter) na Rudeboy (Paulo), lakini hawakufikia kiwango cha mafanikio waliyofurahia na P-Square kama kikundi.
Wakiwa pamoja walitawala muziki wa Nigeria wa Afrobeat kwa miaka mingi na walikuwa moja ya vikundi vya kwanza kusafirisha Afrobeats kwenda sehemu nyingine za bara.