•Mwimbaji huyo mwenye umri wa miaka 32 alibainisha kuwa kuorodheshwa kama mtu tajiri zaidi duniani ni ndoto yake kubwa maishani.
•"Na nawathibitishia kwamba nitakuwa Mtanzania ambaye atawakilisha taifa kuwa Tajiri nambari moja duniani,” alisema
Staa wa muziki wa Bongo, Naseeb Abdul Juma almaarufu Diamond Platnumz amefunguka kuhusu nia yake ya kuwa mtu tajiri zaidi duniani siku moja.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa tamasha la Wasafi Festival 2024, mwimbaji huyo mwenye umri wa miaka 32 alibainisha kuwa kuorodheshwa kama mtu tajiri zaidi duniani ni ndoto yake kubwa maishani.
Diamond alizungumzia dhamira yake ya kutimiza ndoto hiyo yake huku akieleza kuwa yeye ni muumini kuwa kila kitu kinawezekana kwa yeyote.
“Ndoto yangu kubwa katika maisha ni kuwa tajiri namba moja duniani. Ndio ndoto yangu. Na nakuthibitishia kwamba nitakuwa Tajiri kubwa duniani,” Diamond alisema siku ya Jumanne.
Bosi huyo wa WCB aliendelea kuzungumzia jinsi alivyowahi kudhihirisha kuhusu kununua gari la kifahari aina ya Roll Royce, ambalo sasa anamiliki.
“Kwangu mimi naamini kila kitu kinawezekana. Na nawathibitishia kwamba nitakuwa Mtanzania ambaye atawakilisha taifa kuwa Tajiri nambari moja duniani,” alisema.
Pia alizungumza kuhusu mipango yake mipya ya uwekezaji huku tamasha lake la Wasafi Festival 2024 likikaribia kuanza.
Diamond Platnumz ni miongoni mwa wanamuziki wenye viwango vya usanii vya juu, sio tu nchini kwake Tanzania, bali hata katika bara la Afrika.
Pia anaaminika kuwa miongoni mwa wasanii matajiri zaidi barani Afrika kutokana na uwekezaji na mali zake nyingi. Anamiliki lebo kubwa ya muziki, nyumba ya vyombo vya habari, magari na majengo mengi, vito vya gharama kubwa kati ya uwekezaji mwingine na mali.