•Bi Wangui ameomba msamaha kwa kucheka wakati mgeni wake akimdhihaki Pritty Vishy na akabainisha kuwa haikuwa nia yake.
•"Sio na kamwe, na haiwezi kuwa furaha yangu kumdhihaki kimaumbile mtu yeyote na haswa mwanamke," Wangui alisema.
Mtangazaji wa JCM TV Lizz Wangui Muchiri mnamo Jumanne alasiri alinyenyekea na kuomba msamaha kuhusu tabia yake wakati wa mazungumzo yake ya hivi majuzi yenye utata na askofu Benson Gathungu almaarufu Muthee Kiengei.
Mwanahabari huyo alitumia akaunti zake za mitandao ya kijamii kujitetea kufuatia shinikizo na ukosoaji mwingi ambao watumiaji wa mtandao waliibua kuhusu kipindi hicho ambacho kimezua ghadhabu nyingi kutoka kwa Wakenya.
Katika taarifa yake, Bi Wangui aliomba msamaha kwa kucheka wakati mgeni wake akimdhihaki mtayarishaji wa maudhui Pritty Vishy na akabainisha kuwa haikuwa nia yake. Alidai kuwa alicheka kwa sababu ya lafudhi ambayo Kiengei alitumia alipokuwa akimkejeli Vishy na aliyekuwa mpenzi wake Stevo Simple Boy.
"Kwa hili nataka kusema kuwa mimi ni mwanamke kama Pritty Vishy na mimi pia ni mzazi. Sio na kamwe haiwezi kuwa furaha yangu kumdhihaki kimaumbile mtu yeyote na haswa mwanamke. Sikucheka kwa kejeli au kimakusudi lakini ni jinsi lafudhi ambayo mgeni wangu alitumia ilinichekesha,” Bi Wangui alisema.
Aliongeza, “Kwa hivyo ninatoa pole zangu za dhati kwa dada yangu Pritty Vishy wafuasi wangu, na pia kwa yeyote ambaye tulimchukiza kwa matamshi yetu. Kosa ni kwa binadamu na tafadhali pata nafasi ndani ya mioyo yenu mnisamehe ama mtusamehe."
Msamaha wa mtangazaji huyo wa runinga ulikuja baada ya bosi wake Bw Kiengei pia kuomba msamaha kwa Pritty Vishy kutokana na matamshi ya kuudhi aliyotoa wakati wa kipindi cha IHUHUKANIO.
Katika msamaha wake, askofu huyo alikiri kuwa kauli zake ni mbaya na kumtaka mtayarishaji wa maudhui kutafuta nafasi moyoni mwake amsamehe.
“Prity Vishy, samahani sana na nachukua muda huu kukuomba radhi sana kwa kutaja jina lako kwenye kipindi nilichopitia na kukutaja kimakosa, Pata nafasi moyoni mwako kunisamehe kwa kukuhutubia kwa njia isiyo sahihi, njia mbaya,” Kiengei alisema kupitia Facebook.
Mtumbuizaji huyo ambaye pia ni askofu katika kanisa moja maarufu jijini Nairobi aliahidi kutorudia kosa lilelile na akaendelea kumwalika Vishy kwenye kanisa lake.
"Hii haitatokea siku katika zijazo, naichukulia kama kosa langu, Pole dada yangu na karibu sana JCM CHURCH, KANISA LA WATU WOTE," alisema.