Kesi ya 11 dhidi ya Sean 'Diddy' Combs yawasilishwa akiwa bado gerezani

Thalia Graves, anadai Combs na mlinzi wake walimpa dawa za kulevya , kumfunga na kumbaka mnamo 2001, na kurekodi tukio hilo.

Muhtasari

•Diddy kwa sasa yuko chini ya ulinzi wa serikali akisubiri kufikishwa mahakamani kwa tuhuma za ulaghai na utumwa wa ngono.

•Rapa huyo mzaliwa wa Harlem amekana makosa ya jinai.

Image: BBC

Mwanamuziki wa Hip-hop Sean "Diddy" Combs kwa sasa yuko chini ya ulinzi wa serikali akisubiri kufikishwa mahakamani kwa tuhuma za ulaghai na utumwa wa ngono.

Kukamatwa kwake wiki iliyopita mjini New York kulitokea huku kukiwa na msururu wa mashtaka ya unyanyasaji wa kijinsia na unyanyasaji wa kimwili, dhidi yake na mengine yakianzia miaka ya 1990.

Mlalamishi wa 11 na wa hivi punde kujitokeza ni Thalia Graves, anadai Combs na mlinzi wake walimpa dawa za kulevya , kumfunga na kumbaka mnamo 2001, na kurekodi tukio hilo.

Rapa huyo mzaliwa wa Harlem amekana makosa ya jinai.

Kesi ya jinai inahusu nini?

Combs, 54, alikamatwa Jumatatu Septemba 16 katika hoteli ya New York kwa tuhuma za kula njama, kuendesha biashara ya utumwa wa ngono na uhalifu mwingine .

Waendesha mashtaka wa serikali kuu wamemshutumu kwa "kuunda biashara ya uhalifu" ambapo "aliwanyanyasa, kutishia, na kulazimisha wanawake na wengine walio karibu naye kutimiza tamaa zake za kingono, kulinda sifa yake, na kuficha tabia yake".

Walisema Combs ametumia dawa za kulevya, vurugu na nguvu ya hadhi yake "kuwavutia waathiriwa wa kike" katika vitendo vya ngono katika karamu zake zinazoitwa "Freak Offs".

Pia walifichua walikuwa wamepata bunduki, risasi na chupa zaidi ya 1,000 za mafuta wakati wa uvamizi katika nyumba za Combs huko Miami na Los Angeles mnamo Machi.