Mwanamuziki na mjasiriamali mashuhuri wa Kenya Esther Akoth almaarufu Akothee amewashauri kina mama wasio na waume kujitahidi kuwa na mali zao wenyewe.
Katika taarifa ya Jumatatu jioni, msanii huyo mwenye umri wa miaka 43 alibainisha kuwa mwanamke mwenye nyumba yake, lango lake na gari yake mwenyewe ana uhuru zaidi katika maisha yake.
Alibainisha kwamba kuwa na mali humpa mwanamke heshima, si tu kutoka kwake mwenyewe, bali pia anapata kuheshimiwa na wanaume.
“Mwanamke mwenye nyumba yake anajua moyo wake ulipo. Mwanamke mwenye geti lake anajua akili yake ilipo. Mwanamke mwenye gari lake anajua anakoenda. Anaweza kuenda wakati wowote, anaweza pia kurudi wakati wowote,” Akothee aliandika kwenye ukurasa wake wa Facebook.
Aliongeza, "Kina mama wasio na waume, hii ndiyo njia pekee ya kupata heshima sio tu kutoka kwa wanaume bali pia kwako mwenyewe. Nyumba ndogo tamu ambapo unakimbilia kujificha wakati ulimwengu unashuka, mahali ambapo unawaficha watoto wako kutokana na mashida ya ulimwengu.”
Mama huyo wa watoto watano aliwashauri akina mama wasio na waume wafikirie kujipanga kwanza kabla ya kuwafanyia wanaume mambo kwa sababu ya mapenzi.
Alitumia kisa cha ndoa yake iliyovunjika kueleza umuhimu wa mwanamke kuwa na mali yake mwenyewe na kutomtegemea mwanaume yeyote.
“Kabla hujachukua mkopo kujenga biashara ya mtu wako, jenga nyumba yako kwanza, roho. Wacha ipige damu iwache kiherehere, mapenzi baadaye. Si unaona nimewachiwa nyumba ya nguruwe, nguruwe ,kuku, na the rest . Kama ningekuwa naishi kwake je? ningeondoka na nini kama si uhuru bag pekee?” alisema.
Akothee pia aliwataka watu kutoiga njia zake za maisha bali wajifunze kutokana na mienendo yake.
Katika siku za hivi majuzi, mwanamuziki huyo mwenye umri wa miaka 43 anaonekana kufufua uhusiano wake na meneja wake Nelly Oaks. Hii ni baada ya ndoa yake na Denis ‘Omosh’ Schweizer kugonga mwamba ghafla, miezi miwili tu baada ya harusi yao.