Baha azungumzia kuinuka tena kufuatia madai ya matatizo ya kifedha na kamari

Baha alidokeza anashughulikia mambo "Siku moja baada ya nyingine" kwa matumaini ya kuinuka tena.

Muhtasari

•Baha amedokeza kwamba ana matumaini makubwa ya  kuinuka tena baada ya kukabiliwa tuhuma nzito za ulaghai.

•Jumapili asubuhi, alishiriki wimbo  'Mchaguliwa' wa Adasa kuashiria kwamba ana matumaini makubwa katika jitihada zake.

Tyler Mbaya

Muigizaji wa zamani wa kipindi cha Machachari kwenye Citizen TV, Tyler Mbaya almaarufu Baha amedokeza kwamba ana matumaini makubwa ya  kuinuka tena baada ya kukabiliwa tuhuma nzito za ulaghai.

Hivi majuzi, muuguzi mmoja Mkenya anayeishi Marekani aliibua madai kwamba muigizaji huyo  alimlaghai pesa.

Nurse Judy, kama anavyojitambulisha kwenye mitandao ya kijamii, alidai kuwa Baha alimtafuta akimuomba msaada huku akieleza kwamba  alikuwa anakabiliwa na matatizo ya kifedha na alikaribia kufungiwa nyumba. Alidai Baha alimuomba dola 400  lakini akamtumia dola 150 pekee ambapo aliendelea kumuomba zaidi.

“Baada ya kumtumia dola 150 ambazo hata hakuzithamini, alianza kutuma  sauti za huruma, akizungumzia kutokuwa na wazazi na marafiki wa kugeukia isipokuwa nesi Judy cheeii. Aliendelea kupiga simu, nikawa naudhika. Nilienda kwenye ukurasa wa mkewe ili kuangalia kama huenda akaunti yake ilidukuliwa na labda alitangaza. Lakini nilipofika huko nililazimika kwenda DM," Judy alisema .

Kufuatia madai hayo, Baha alikiri kwamba hayuko sawa na kueleza kuwa anashughulika katika juhudi za kutatua mambo.

"Siko sawa, ninaifanyia kazi," alisema Ijumaa.

Aliendelea kufichua kuwa anauza akaunti yake ya Instagram na ya TikTok, labda ili kusuluhisha matatizo yake ya kifedha.

Muigizaji huyo mwenye umri wa miaka 23  alidokeza anashughulikia mambo  "Siku moja baada ya nyingine" kwa matumaini ya kuinuka tena.

Siku ya  Jumapili asubuhi, alishiriki wimbo  'Mchaguliwa' wa Adasa kuashiria kwamba ana matumaini makubwa katika jitihada zake.

"Kazi inaendelea..," Baha alisema kwenye video hiyo ambayo alichapisha kwenye ukurasa wake wa Instagram.

Katika ufichuzi wake siku ya Ijumaa, Nurse Judy alidai kuwa mpenziwe Baha, Georgina Njenga alifutilia mbali madai ya kufurushwa kutoka kwa nyumba yao ya kupanga na akamfichulia kuwa muigizaji huyo anakabiliwa na tatizo la kamari. Georgina aidha alibainisha kwamba amekuwa akigharamia bili zote.

"Ana tatizo la kamari lakini kama kuna chochote hakukopa pesa ili kutusaidia kwa lolote, pengine kwake," ujumbe ambao Judy alidai ulitoka kwa Georgina ulisomeka.

Judy alidai kwamba watu wengine kadhaa huko Marekani pia walidai kupokea maombi sawa kutoka kwa mwigizaji huyo.

Aidha, Jumamosi ilibainika kwamba muigizaji huyo na mzazi mwenzake, Georgina Njenga wameacha kufuatiliana kwenye mtandao wa Instagram, dokezo kwamba heunda mambo sio mazuri kabisa nyumbani.