Mwanamuziki wa Bongo Rajab Abdul Kahali almaarufu Harmonize amezungumza kuhusu suala la yeye kumkabidhi bosi wake wa zamani Diamond Platnumz tuzo moja kati ya matatu aliyoshinda katika hafla ya kutuza wasanii bora nchini Tanzania.
Akihutubia waandishi wa Habari katika ukumbi wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam, Harmonize alisema alihisi bosi huyo wa WCB anafaa zaidi ya tuzo moja alilopata kwa mchango wake mkubwa katika muziki waTanzania.
Mmiliki huyo wa lebo ya Konde Gang pia alisema hatua yake ni kielelezo cha ushirikiano mzuri miongoni mwa wanamzuki wa Bongo.
"Hizi tuzo zinaenda mbali. Hata watu wa mataifa ya mbali wakiona hivo, tunashinda matuzo na kupeana, ni jambo nzuri sana. Wanaona tasnia ya muziki ya Tanzania inakua na kuna ushirikiano mzuri," Harmonize alisema.
Harmonize afichua sababu za kumpa Diamond tuzo yake
Harmonize alitambua ubabe wa bosi huyo wake wa zamani katika muziki. Alikiri kwamba isingalikuwa Diamond, labda yeye hangewahi kufanikiwa kimuziki.
"Nilihisi kwamba anafaa zaidi. Pongezi kwa serikali kwa kutengeza tuzo ya heshima na kumpatia yeye na Bi Kidude. Inawezekana isipokuwa ni yeye msingenifahamu mimi. Sisi ni familia," Harmonize alisema.
Katika hafla ya kutuza wasanii bora Tanzania iliyoandaliwa Jumamosi usiku, Harmonize alimwalika Diamond jukwaani na kumpatia tuzo ya 'Msanii bora wa mwaka' ambayo alikuwa amekabidhiwa yeye.