AMBER RAY VS AMIRA

Usinisulubishe kwa kuwa mke wa pili! Amber Ray amuonya Amira dhidi ya kuingilia maisha yake

Amber Ray amemtaka Amira kumkubali na kumheshimu kama mke mwenza.

Muhtasari

•Amber Ray amemwambia Amira ambaye ni mke wa kwanza kuwa haikuwa pendekezo lake kwa Jamal kumfanya mke wa pili.

•Mwanasoshalaiti huyo alimkosoa Amira kwa madai kuwa anatumia mitandao ya kijamii kutafuta huruma kutoka kwa watu.

Amber Ray, Jamal Rohosafi, Amira
Amber Ray, Jamal Rohosafi, Amira
Image: Instagram

Baada ya vita kubwa ya maneno iliyoshuhudiwa kati ya mabibi wawili wa mwanabiashara, Jamal Rohosafi usiku wa Jumanne, Amber Ray ametokea kumkashifu mke wa kwanza kwa kile anasema ni kumsulubisha kwa kuwa mke wa pili.

Amber Ray amemwambia Amira ambaye ni mke wa kwanza kuwa haikuwa pendekezo lake kwa Jamal kumfanya mke wa pili.

Kupitia ujumbe alitoa kwenye mtandao wa YouTube, Amber Ray amemtaka Amira kumkubali na kumheshimu kama mke mwenza.

"Usijaribu kunisulubisha kwa kuwa mimi ni mke wa pili. Najua barani Afrika ni ngumu watu kukubali wake wa pili lakini hivyo ndivyo hali ilivyo. Haya yanafanyika siku hizi. Ingawa unakataa kugawana, tunagawana , iko hivo" Amber Ray alisema.

Mwanasoshalaiti huyo alimkosoa Amira kwa madai kuwa anatumia mitandao ya kijamii kutafuta huruma kutoka kwa watu.

Amemtaka mwenzake wa kwanza kusita kuingilia maisha yake na kumuacha aishi anavyotaka mwenyewe.

"Kabla niolewe na Jamal nilikuwa naishi maisha yangu jinsi naishi leo. Nilikuwa navaa jinsi navaa leo. Leo naweza tamani kuvaa nguo refu kesho nijiskie kuvaa leso  na niko sawa na watu ambao wanahusika katika maisha yangu wanajua hayo na wako sawa vile. 

Kwa hivyo usijaribu kuja maishani mwangu na ufanye kuwa ni sharti niishi kwa namna fulani kuwa mke wa pili eti kwa kuwa wewe ni mke wa kwanza na unavaa hii. Wacha kila mtu aishi maisha yake" Ray alisema.

Amemuagiza kutojihusisha sana na maisha yake na waheshimiane.

"Kila mtu aangalie kwake, afagie kwake.. ni lazima ujiheshimu kwanza ndio nikuheshimu pia. Namna unavyokuja kwanga inaamua sana vile nitakujibu.. Pia mimi ni binadamu na mimi ni wa mitaani, nitapigana pia. Siko hapa kukanyangwa" Alisema.

Ray alisema kuwa anajivunia kitendo cha bwanake kuweka wazi  uhusiano wao na  kukubali kumtangaza kama bibi wake. Alisema kuwa si yeye alimlazimisha Jamal kumuoa. 

Wawili hao walitumbuiza Wakenya na vita ya maneno ambayo Amber Ray alirekodi na konyesha mashabiki wake kwenye mtandao wa Instagram usiku wa Jumanne.

Amesema kuwa si yeye alisababisha vita ile ila ni Amira alikuja kumshambulia akiwa kwake na hasira ilipomzidia akaamua kujipigania.