Sonko asihi gavana Mutua na Lilian wasameheane, akemea msanii anayehusishwa na sakata hiyo

Sonko hakusaza nyuma 'msanii mmoja ambaye ametajwa sana mitandaoni na kuhusishwa na sakata hiyo na kusema kuwa ingekuwa imemtendekea yeye angechukua hatua kali mikononi

Muhtasari

•Sonko amewasihi wawili hao kusameheana na kusahau chochote ambacho kiliibua mzozo kati yao na kusema kuwa hayo ni mambo ya familia

•Mwanasiasa huyo amewaomba waandishi wa habari kukaa mbali na maisha ya kibinafsi ya gavana Mutua na kusema kuwa mzozo kwa familia ni jambo la kawaida.

•Amewaomba Mutua na Lilian kutoskiza maneno ya watu na kuzungumzia maneno yao kama familia.

Image: HISANI

Aliyekuwa gavana wa Nairobi Mike Mbuvi Sonko ameshauria gavana Alfred Mutua na mkewe Lilian Ng'ang'a kushiriki mazungumzo na kutafuta suluhu juu ya kile kilichofanya watengane.

Kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii, Sonko amewasihi wawili hao kusameheana na kusahau chochote ambacho kiliibua mzozo kati yao na kusema kuwa hayo ni mambo ya familia.

Kulingana na mwanasiasa huyo asiyepungukiwa na drama, wawili hao wamekuwa pamoja kwenye mahusiano kwa zaidi ya mwongo mmoja na kwa hivyo hawafai kupatia shetani nafasi katika ndoa yao.

"Lilian wewe ni mwanamke jasiri na endelea kuwa jasiri haswa kwa sasa ambapo unapitia wakati mgumu. Tunasema kuwa kando ya kila mwanaume kuna mwanamke, umekuwa na Dr Alfred Mutua tangu 2011 wakati ambapo nilichaguliwa kama mbunge miaka 15 iliyopita. Kumaanisha umekuwa naye hata kabla akuwe gavana. 

Ombi langu kwenu ni msameheane na  msahau yaliyotokea maishani kati yenu na mkubaki kuwa shetani ni muongo na hana nafasi maishani mwenu." Sonko alisema.

Mwanasiasa huyo pia amewaomba waandishi wa habari kukaa mbali na maisha ya kibinafsi ya gavana Mutua na kusema kuwa mzozo kwa familia ni jambo la kawaida.

"Wanablogu wenzangu, tafadhali kaeni mbali na maisha ya gavana Alfred Mutua. Kukula na kukuliwa ni kawaida na ni sehemu ya maisha. Hata nyinyi mabibi zenu wanakulwa tu vile munakulana nje lakini hawawezi kubali mjue vile tu nyinyi hamkubali wao wajue mukikulana nje"  Sonko aliandika.

Hata hivyo amewaomba Mutua na Lilian kutoskiza maneno ya watu na kuzungumzia maneno yao kama familia.

"Hii ni kuwahusu nyinyi wawili kama familia kwa hivyo wacha watu waongee mchana lakini wote wataenda kulala usiku na maisha yatasonga mbele.  Nawaomba msameheane kwani hii ni mambo ya kidunia" Sonko aliambia Mutua na Lilian.

Sonko hakusaza nyuma 'msanii mmoja ambaye ametajwa sana  mitandaoni na kuhusishwa na sakata hiyo na kusema kuwa ingekuwa imemtendekea yeye angechukua hatua kali mikononi.

"Na wewe msanii jipe shughuli ingekuwa ni ati tumekosana na bibi yangu alafu siku za kwanza baada ya kutengana unadunda naye kuniumiza hiyo 'sausage' yako naweza kuikata vipande vipande na nijipeleke kwa kituo cha polisi" Sonko alisema.

Siku ya Jumapili gavana Mutua na Lilian Nganga walitangaza kuwa walifanya maamuzi ya kutamatisha ndoa yao miezi miwili iliyopita.