Samidoh hawezi kuacha mkewe kwa sababu yangu - Karen Nyamu

"Aliniachia niamue ninachotaka lakini sasa, naweza kusema yuko sawa."

Muhtasari

Kuhusu jinsi alivyo toa habari hiyo kwa baba yake mtoto, Karen alisema, alingoja hadi alipomtembelea.

Karen anasema Biblia ni mwongozo wake na kwa hivyo anaelewa kuwa ni Mungu anayetoa watoto.

Mwanasiasa Karen Nyamu Picha: RADIO JAMBO
Mwanasiasa Karen Nyamu Picha: RADIO JAMBO

Mwanasiasa Karen Nyamu anatarajia mtoto wake wa pili na mwanamziki wa Mugiithi Samidoh lakini hatarajii mwanamziki huyo kuachana na mkewe ambaye ana watoto wake wawili.

Akiongea kwenye Jeff Kuria TV, Karen alisema habari za ujauzito zilimshtua. Alikuwa na mawazo mengi kwa miezi miwili baada ya kuthibitisha kwamba alikuwa na mimba.

"Mwanangu ana miezi 10 sasa, imekuwa vyema kuona watoto wangu wakikua. Mimba hii ya sasa haikupangwa," alisema.

"Nilipata vifaa vya kujipima na nikajipima nikiwa chooni ili kudhibitisha kwani nilikuwa nimekosa hedhi yangu na nilijiona mjinga kwani haikupangwa, ikizingatiwa tunaelekea kwenye msimu wa kampeni... Sikutaka kuamini. Namaanisha wakati ulikuwa mbaya. "

Aliongezea, "Watoto wangu wengine wawili, nilifurahi sana juu ya ujauzito wao, lakini huyu nilikuwa na mawazo. Furaha ilijiri baada ya kupiga picha ya mimba hiyo. Sasa ni jambo zuri."

Karen anasema Biblia ni mwongozo wake na kwa hivyo anaelewa kuwa ni Mungu anayetoa watoto.

"Ndio, nilisoma Biblia na watoto ni zawadi Zake. Tunajua watu ambao wameoa lakini wanajitahidi kupata watoto, kwa hivyo niko sawa."

Kuhusu jinsi alivyo toa habari hiyo kwa baba yake mtoto, Karen alisema, alingoja hadi alipomtembelea.

"Aliniachia niamue ninachotaka lakini sasa, naweza kusema yuko sawa."

Alipoulizwa kwa nini Samidoh na sio mtu mwingine, Karen alisema wote ni watu wazima.

"Watu huniita mnyakuzi wa mume lakini namjua vizuri, hawezi kuiacha familia yake. Mkewe kwa sasa anajua kuwa sina nia ya kuja kati yao."

Akizungumzia madai kwamba Samidoh alimpiga, Karen alisema alikuwa amefadhaishwa.

"Nilikuwa na wasiwasi sana, nilikuwa na uchungu na hasira. Binti yangu hakushuhudia tukio hilo kwani alikuwa amefunga mlango lakini nilikuwa na hasira," alisema.

"Nilikwenda kwenye Instagram kama njia ya kulipiza kisasi. Nilikuwa nimeudhika kwani ukiniuliza mmoja wa watu wazuri zaidi ambao nimekutana nao, ni yeye."

Wakati huo kwa sababu ya hasira, alikuwa ametishia kuchukua hatua za kisheria dhidi ya Samido.