"Wanasema nimemroga, nawe kamroge mumeo pia" Nyota Ndogo anunuliwa gari na mumewe mzungu kama poza

Muhtasari

•Mama huyo wa watoto wawili amemshukuru Mola kwa kumpatia mume ambaye anamsikiza kila wakati na kumjali huku akisuta wanaosema kuwa amemroga Mholanzi huyo.

•Nyota Ndogo alimwambia mumewe kuwa zawadi ile ingekuwa poza kwa kuumiza moyo wake alipokuwa amemtema na kumnyamazia mapema mwaka huu.

Image: INSTAGRAM// NYOTA NDOGO

Mwanamuziki mashuhuri toka Pwani Mwanaisha Abdalla almaarufu kama Nyota Ndogo ni mwenye bashasha isiyoelezeka baada ya kununuliwa gari na mumewe.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Nyota Ndogo alionyesha video ya gari aina ya BMW ambayo alinunuliwa na mumewe Henning Neilsen.

Mama huyo wa watoto wawili amemshukuru Mola kwa kumpatia mume ambaye anamsikiza kila wakati na kumjali huku akisuta wanaosema kuwa amemroga Mholanzi huyo.

"Kwanza kabisa nataka kutoa Shukran zangu kwa MUNGU.. Ahsante kwa MUNGU kwa kunipa mume ambae nikikohoa tu anasikiza. Haya wanasema nimemroga haya na wewe kamroge mumeo pia akusikilize kama munaona kuroga ndio kuskizwa" Alisema Nyota Ndogo huku akionyesha gari lake mpya.

Wiki iliyopita msanii huyo alikuwa ameomba mumewe amnunulie gari ambalo alisema angetumia kufanya ziara zake za muziki na kuhudumia wateja wa biashara yake ya vyakula ya  @nyotandogo_jikoni.

Nyota Ndogo alimwambia mumewe kuwa zawadi ile ingekuwa poza kwa kuumiza moyo wake alipokuwa amemtema na kumnyamazia mapema mwaka huu.

Kidogo nilikuwa mwenye huzuni nikamuuliza mbona amenifanya nikalia hivyo alafu akasema pole, Ungependa nikufanyie nini huzuni iondoke?. Alafu hapa nikajibu. Mpenzi wangu  unajua hii Gari yangu nataka iwe ya @nyotandogo_jikoni. Sasa utanipoza ukininunulia Sasa Gari ya nyota ndogo ya kwenda show. Alafu akakubali. Sasa tungoje" Nyota Ndogo aliandika kwenye ukurasa wake wa Instagram siku chache zilizopita.

Ama kweli hayawi hayawi huwa, baada ya kusubiri kwa siku chache hatimaye Neilsen ambaye kwa sasa yuko nchini kumtembelea mpenziwe alitimiza ahadi yake na kumpoza Nyota Ndogo kwa kumnunulia gari kama alivyotaka.