Nonini amtetea mwanamuziki mwenzake Juliani kufuatia madai kuwa amefilisika

Muhtasari

•Baadhi ya wanamitandao wamekuwa wakikosoa hatua ya Lilian Ng'ang'a kumtema gavana Alfred Mutua na kujitosa kwenye wahusiano na Juliani wakidai kuwa alitoka kwa kasri na kuenda kuishi kwa kibanda.

•Mwanamuziki huyo wa nyimbo za genge amedai kwamba Juliani ni  miongoni mwa wasanii wenye mafanikio makubwa nchini huku akieleza kuwa kuna wakati alikuwa anapata kipato cha shilingi milioni 20 kila mwaka.

•Nonini amewasihi Wakenya kuacha kufikiria kuwa Juliani amefilisika kwa kuwa anavalia mavazi ya kawaida na amefunga nywele ilhali aliyekuwa mume wa mpenzi wake anavalia suti.

Image: INSTAGRAM

Mwanamuziki Hubert Mbuku Nakitare almaarufu kama Nonini amejitokeza kutetea mwanamuziki mwenzake Juliani ambaye wengi wamekuwa wakimuita fukara hohehahe.

Baadhi ya wanamitandao wamekuwa wakikosoa hatua ya Lilian Ng'ang'a kumtema gavana Alfred Mutua na kujitosa kwenye wahusiano na Juliani wakidai kuwa alitoka kwa kasri na kuenda kuishi kwa kibanda.

Hata hivyo, kulingana na Nonini Lilian hakuacha bwenyenye na kuenda kuchumbia fukara kwani  mzaliwa huyo wa Dandora hajafilisika kama wanavyodai wanamitandao wengi.

Nonini  amelinganisha kipato cha wasanii na wanasiasa akidai kuwa wanamuziki wengi  kama vile Juliani hutia bidii kubwa kazini mwao ili wajikimu kimaisha tofauti na viongozi ambao hupokea mshahara kila mwisho wa mwezi.

"Inachekesha jinsi wanamitandao wanafikiria kuwa Juliani amefilisika. Ni wazi kuwa wanamuziki wengi wamejiajiri na wanatia bidii kupata pesa sio kama gaana ambaye analipwa kila mwezi na marupurupu mengine  lakini kwa kipindi cha mwongo mmoja ambao umepita  jamaa huyu (Juliani) amekuwa akiangaziwa sana na yeye ni miongoni wa wasanii wenye mafanikio makubwa ya kifedha kutoka kizazi chetu" Nonini alieleza kupitia ukurasa wake wa Facebook.

Kulingana na Nonini, wengi wamekuwa wakimuita Juliani maskini kwa kuwa huwa anapendelea sana kujihusisha na mahali alikotoka.

Hata hivyo mwanamuziki huyo wa nyimbo za genge amedai kwamba Juliani ni  miongoni mwa wasanii wenye mafanikio makubwa nchini huku akieleza kuwa kuna wakati alikuwa anapata kipato cha shilingi milioni 20 kila mwaka.

"Jamaa huyu (Juliani) alikuwa anatengeneza shilingi milioni 20 kila  mwaka kutokana na muziki wake. Wanamitandao wengi wanamuita fukara kwa sababu huwa anajihusisha na mizizi yake. Jamaa huyu ako na mradi ambao amegharamia mwenyewe Dandora" Alisema Nonini.

Nonini amewasihi Wakenya kuacha kufikiria kuwa Juliani amefilisika kwa kuwa anavalia mavazi ya kawaida na amefunga nywele ilhali aliyekuwa mume wa mpenzi wake anavalia suti.

Mwanamuziki huyo amesema kuwa dhana hiyo ndiyo ina fanya Wakenya wengi waibiwe na watapeli waliovalia suti.