"Kutaneni mjadili ninachofaa kufanya" Lilian Ng'ang'a awakemea vikali wakosoaji

Muhtasari

•Lilian amewaita wanaosumbuliwa na jinsi anaishi maisha watu pweke, wenye machungu na wasio na matumaini maishani.

•Amewaagiza wakosoaji wake wapange mkutano ambao ajenda kuu itakuwa kujadili jinsi anafaa kuishi maisha yake kisha kuwasilisha mapendekezo baada ya sikukuu ya utamaduni.

•Mpenzi huyo wa Juliani amewataka wakosoaji kueleza jinsi chuki ambayo wameonyesha mitandaoni imeathiri maisha yake.

Image: INSTAGRAM// LILIAN NG'ANG'A

Aliyekuwa mke wa gavana wa Machakos Alfred Mutua, Bi Lilian Ng'ang'a ako na ujumbe wazi kwa wakosoaji wake.

Lilian ambaye kwa sasa anafurahia mahusiano mapya na mwanamuziki mashuhuri Julius Owino almaarufu kama Juliani amewataka wakosoaji wake kuwashwa na pilipili wanayoila wenyewe.

Kupitia ukurasa wake rasmi wa Instagram, Bi. Lilian amewaagiza wakosoaji wake wapange mkutano ambao ajenda kuu itakuwa kujadili jinsi anafaa kuishi maisha yake kisha kuwasilisha mapendekezo baada ya sikukuu ya utamaduni.

Lilian amewaita wanaosumbuliwa na jinsi anaishi maisha watu pweke, wenye machungu na wasio na matumaini maishani.

"Kwa kuwa hii ni wikendi refu, watu hao wote wasio na matumaini, walio pweke na wenye machungu ambao wanasumbuliwa na jinsi nafaa kuishi  maisha yangu wanafaa wakutane wajadili ninachofaa kufanya na kuwasilisha ripoti ya mapendekezo siku ya Jumanne" Lilian aliandika kwenye ukurasa wake wa Instagram siku ya Jumamosi.

Mpenzi huyo wa Juliani amewataka wakosoaji kueleza jinsi chuki ambayo wameonyesha mitandaoni imeathiri maisha yake.

"Je, kuonyesha ujinga na upumbavu wenu mitandaoni kumenisaidiaje kwenye njia ya kuwa bora. Onyesha mifano" Alisema Lilian.

Baadhi ya wanamitandao wamekuwa wakimkosoa sana kufuatia uamuzi wake wa kumtema gavana Mutua na kujitosa kwenye mahusiano na Juliani.

Uamuzi huo ambao alidhihirisha wazi takriban miezi miwili iliyopita uliibua gumzo mitandaoni huku wengi wakionekana kushangazwa na hatua hiyo.

Hata hivyo Lilian na kipenzi chake kipya Juliani wameendelea kufurahia mapenzi yao na kufungia kelele za wakosoaji masikio.