'Tutajiburudisha na kipenzi usiku kucha,' Akothee asherehekea kuondolewa kwa kafyu

Muhtasari

•Akothee alieleza kwamba itabidi tuhame mitaani kwani kuanzia sasa yeye pamoja na mpenzi wake watapiga sherehe usiku kucha.

•Hata hivyo mwanamuziki huyo amejitokeza kulalamikia hatua ya serikali ya kuendeleza masharti mengine licha ya kuondolewa kwa kafyu.

Image: INSTAGRAM// AKOTHEE

Hatua ya rais ya kuondoa kafyu ya kitaifa ilipokewa kwa shangwe na vigelegele na kikundi kikubwa cha wananchi ambao walikuwa wamechoka kulazimika kuingia kwa nyumba kabla ya saa nne usiku.

Wakenya wengi haswa wanaopenda kujiburudisha usiku walisherehekea habari hizo kwenye mitandao ya kijamii.

Siku ya Jumatano rais Kenyatta aliagiza amri yakutotoka nje usiku iondolewe mara moja na kutangaza raia waruhusiwe kuingia kwa nyumba wakati wowote.

"Kulingana na madaraka ambayo nimepatiwa kama rais, naamuru na kuelekeza kwamba kafyu ya kitaifa ya kutoka usiku hadi asubuhi ambayo imekuwepo tangu tarehe 27 Machi 2020 iondolewe mara moja" Rais aliamuru.

Miongoni mwa walioshindwa kuzuia furaha yao kutokana na tangazo hilo ni mwanamuziki mjasiriamali mashuhuri nchini Esther Akoth almaarufu kama Akothee..

Muda mfupi baada ya habari kuhusu kuondolewa kwa kafyu kuvunja vichwa vya habari mama huyo wa watoto watano alipakia video kwenye mtandao wa Instagram ambayo ilionyesha akisakata densi na mpenzi wake Nelly Oaks.

Chini ya video hiyo Akothee alieleza kwamba itabidi tuhame mitaani kwani kuanzia sasa yeye pamoja na mpenzi wake watapiga sherehe usiku kucha.

"Mtahama kutoka mitaa hii, ni mimi na @nellyoaks. Hakuna curfew tena baby. Rais akiondoa kafyu ni mimi na wewe mpenzi usiku kucha " Akothee alisema.

Vile vile msanii huyo alipakia video nyingine iliyoonyesha akimbusu Oaks huku wakiwa wanajiburudisha kwa vinywaji.

Hata hivyo mwanamuziki huyo amejitokeza kulalamikia hatua ya serikali ya kuendeleza masharti mengine licha ya kuondolewa kwa kafyu.

"Serikali inafaa kueleza haswa ni kafyu gani iliyoondolewa. Kuondoa kafyu kwa masharti kutahatarisha tu maisha ya Wakenya. Hebu fikiria unajaribu kubishana na polisi wakati umelewa kuhusu mambo fulani na yeye anafanya tu kazi yake!" Akothee alilalamika kupitia ukurasa wake wa Instagram.

Wasanii wengine ambao walionekana kuridhishwa na kuondolewa kwa kafyu ni pamoja na rapa Khaligraph Jones, aliyekuwa mpenzi wa Diamond Tanasha Donna ,mchekeshaji Churchill  kati ya wengine.