"Binti yangu alishutumiwa kuwa Illuminati, walimu waliambia wanafunzi wasimkaribie" Akothee asimulia jinsi walimu walinyanyasa mabinti wake juu ya umaarufu wake

Muhtasari

•Mama huyo wa watoto watano amefichua kwamba walimu wa  bintiye mdogo Fancy Makadia waliwahi kuambia wanafunzi wengine wakae mbali naye baada ya kumshtumu kuwa mfuasi wa Illuminati, jambo ambalo lilimfanya aanze kuanguka mitihani.

•Akothee pia amefichua kwamba walimu wa Vesha na Rue walikuwa na mazoea ya kuwakejeli mabinti wake  kuwa mama yao amepagawa na hana mwelekeo.

Image: INSTAGRAM// AKOTHEE

Mwanamuziki na mfanyibiashara mashuhuri Esther Akoth almaarufu kama Akothee amefunguka kuhusu jinsi walimu walivyonyanyasa mabinti wake watatu waliokuwa shuleni.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Akothee amedai kwamba walimu wa mabinti wake Vesha Okello, Rue Baby na Fancy Makadia  waliwanyanyasa kwa sababu ya umaarufu wake.

Amesema kwamba umaarufu umetia watoto wa watu mashuhuri taabani huku akieleza kwamba jambo hilo linawapea wazazi kama yeye wasiwasi mkubwa 

Mama huyo wa watoto watano amefichua kwamba walimu wa  bintiye mdogo Fancy Makadia waliwahi kuambia wanafunzi wengine wakae mbali naye baada ya kumshtumu kuwa mfuasi wa Illuminati, jambo ambalo lilimfanya aanze kuanguka mitihani.

"Umaarufu unatishia wazazi sana. Binti yangu @fancy_makadia alishutumiwa kuwa mfuasi wa Illuminati na waalimu wakaagiza wanafunzi wengine wakae mbali na yeye. Alianza kuanguka shuleni na angelia sana wakati shuleni zingefunguliwa" Akothee alisimulia.

Msanii huyo mwenye umri wa miaka 41 amesema kwamba mateso ambayo bintiye alikuwa anapitia katika shule hiyo yalifanya amhamishe na kumpeleka kwingine.

Akothee pia amefichua kwamba walimu wa Vesha na Rue walikuwa na mazoea ya kuwakejeli mabinti wake  kuwa mama yao amepagawa na hana mwelekeo.

" Mabinti wangu @rue.baby na @veshashaillan walikuwa na mwalimu ambaye angewaambia kuwa mama yao hana  mwelekeo. Angewauliza kama mimi niko timamu!" Alisema Akothee.

Alidai kwamba kunaye mwalimu ambaye angebadilisha sura punde tu baada ya kuwaona mabinti wake pale shuleni.

Hata hivyo amesema kwamba anajivunia kuona watoto wake walimaliza shule hadi chuo kikuu bila kuwa na visa vya utovu wa nidhamu ama ujauzito.

"Mwalimu wa pili wa kike angekasirika punde tu baada ya kuona watoto wangu. Mimi ni mzazi ambaye sikuwahi kosa kuhudhuria mikutano ya wazazi shuleni. Watoto wangu walimaliza shule hadi chuo kikuu bila ujauzito ama utou wa nidhamu. Mtoto wa mwalimu huyo alikataa shule" Akothee alisema.

Mwanamuziki huyo alikuwa anazungumzia kisa ambapo mwigizaji  mashuhuri wa Nigeria Mercy Johnson anadai kwamba bintiye aliteswa shuleni na mwalimu aliye na chuki dhidi yake.