Gloria Muliro aolewa tena miaka 6 baada ya kumpa talaka aliyekuwa mumewe, Pastor Omba

Muhtasari

•Muliro alifunga pingu za maisha na Evans Sabwami siku ya Jumamosi jijini New York, Marekani katika hafla iliyohudhuriwa na wageni wachache.

•Mnamo mwaka wa 2015 mwanamuziki huyo alimpa talaka aliyekuwa mume wake, Pastor Omba huku akimshutumu  kuwa alikuwa anatoka nje ya ndoa

Image: FACEBOOK// GLORIA MULIRO

Miaka sita baada ya ndoa yake ya kwanza kufika hatima, mwanamuziki mashuhuri wa nyimbo za injili Gloria Muliro hatimaye amevishwa pete na mpenzi wake mpya.

Muliro alifunga pingu za maisha na Evans Sabwami siku ya Jumamosi jijini New York, Marekani katika hafla iliyohudhuriwa na wageni wachache.

Wanandoa hao wawili walitangaza hatua hiyo kupitia kurasa zao za mitandano ya kijamii.

"Hatimaye, hatimaye.. Harusi yangu ya majira ya majani kupukutika" Muliro alitangaza kwenye ukurasa wake wa Instagram.

Haya yanajiri takriban miezi tisa baada ya staa huyo wa muziki wa injili kumtambulisha mpenzi wake hadharani kwa mara ya kwanza kupitia mitandao ya kijamii.

Muliro alimtambulisha raia huyo wa Marekani mnamo siku ya Valentines huku akimtaja kama mwanaume wa maana zaidi maishani mwake na rafiki yake wa dhati.

"Siku ya furaha ya Valentines rafiki wangu wa dhati, mwanaume wa maana zaidi maishani mwangu, na sababu yangu kusherehekea siku hii. Nakupenda sana, Ev" Bi Muliro alisema.

Sabwami ni mhandisi na mhubiri nchini Marekani.

Mnamo mwaka wa 2015 mwanamuziki huyo alimpa talaka aliyekuwa mume wake, Pastor Omba huku akimshutumu  kuwa alikuwa anatoka nje ya ndoa. Wawili hao walikuwa wamekaa kwa ndoa kwa kipindi cha miaka sita.