Miss Morgan asimulia alivyojipata kwa taaluma ya uigizaji kwa njia ya bahati punde baada ya kumaliza kidato cha nne

Muhtasari

•Alisema kwamba alianza kuigiza alipokuwa karibu kumaliza masomo ya sekondari akikusudia kuwa anapata nafasi ya kutoka nje ya shule

•Waruinge alifichua kwamba alipata kazi yake ya kwanza ya kuigiza kwenye tangazo punde baada ya kukamilisha kidato cha nne.

•Alifichua kwamba alilipwa robo milioni kufanya tangazo hilo na kutokana na furaha kubwa aliyopata akaamua kupongeza mwili wake kwa vyakula tamutamu.

Image: INSTAGRAM// ANGEL WARUINGE

Mwigizaji wa kitambo wa Tahidi High Angel Waruinge amekiri kwamba haikuwa ndoto yake kujiunga na usanii.

Akiwa kwenye mahojiano na Tempire TV hivi karibuni, Waruinge ambaye aliigiza kama Miss Morgan alifichua kwamba alipokuwa anakua alijihusisha zaidi kwa michezo wala sio sanaa.

Alisema kwamba alianza kuigiza alipokuwa karibu kumaliza masomo ya sekondari akikusudia kuwa anapata nafasi ya kutoka nje ya shule.

"Sikudhani ningekuwa mwigizaji. Kuigiza ilikuja tu kibahati. Nilipokuwa nakua nilikuwa mashuhuri shuleni kwani nilishiriki kwa mijadala lakini nilishiriki zaidi kwa michezo. Nilikuwa naogelea, niliwakilisha shule na taifa langu. Nilijiunga na michezo ya kuigiza nikiwa katika kidato cha nne.. Nilikuwa mzuri kwa masomo lakini sikung'ang'ana" Waruinge alisema.

Waruinge alifichua kwamba alipata kazi yake ya kwanza ya kuigiza kwenye tangazo punde baada ya kukamilisha kidato cha nne.

Alisimulia alivyohudhuria majaribio ya vipawa baada ya kuona tangazo bila kukusudia angeweza kuchukuliwa.

"Nilipomaliza kidato cha nne nilianza kupata mafunzo ya Kifaransa. Siku moja mwalimu alikosa kuja darasani. Ilikuwa mwendo wa saa nane na lazima ningesubiri babangu atoke kazini saa kumi na moja ili tuende naye nyumbani. Nilishindwa nifanye nini na hapo nikaona tangazo kwamba kulikuwa majaribio ya vipawa ili kutambua waigizaji wa tangazo. Niliamua kwenda kupitisha muda pale. Kulikuwa na watu wengi pale. Nilikuwa mrembo sana, wakaniuliza umri wangu. Kwa bahati nilipata ile kazi" Alisimulia Bi Waruinge.

Mwigizaji huyo alifichua kwamba alilipwa robo milioni kufanya tangazo hilo na kutokana na furaha kubwa aliyopata akaamua kupongeza mwili wake kwa vyakula tamutamu.

"Siku 21 baada ya kuigiza kwa tangazo hilo nilipata shilingi 250, 000 kwa akaunti yangu. Nilishangaa sana. Nilienda nikanunua soseji nyingi na viazi (chips). Pesa hazikuwa zinaisha. Hata sikuwa nimepokea matokeo ya mtihani wangu" Alisimulia Waruinge.

Alieleza kwamba jambo hilo lilimpatia motisha wa kuendelea na uigizaji na akaanza kuhudhuria majaribio ya vipawa.