Onyesho la tatu la shoo ya Wife Material lilimgharimu Eric Omondi zaidi ya Milioni 8:- Butita afichua

Muhtasari

•Butita alieleza kuwa Omondi alitumia zaidi ya milioni nane ili kufanikisha shoo hiyo ambayo ilikamilika siku ya Ijumaa.

•Alipoulizwa kwa nini shoo ile ilichukua muda mfupi tu ilhali pesa nyingi zilitumika Butita alieleza kuwa ilikuwa ghali  mno kuifanikisha.

•Mchekeshaji huyo pia  alisema kwamba alikuwa ameonya Omondi dhidi ya kununua nyumba ambayo inadaiwa kumgharimu milioni 141

Image: INSTAGRAM// ERIC OMONDI

Mwandishi na mwelekeza filamu Eddie Butita amefichua kwamba onyesho la tatu la shoo ya Wife Material lilimgharimu mchekeshaji Eric Omondi kitita kikubwa sana cha pesa.

Alipokuwa kwenye mahojiano na Mungai Eve, Butita alieleza kuwa Omondi alitumia zaidi ya milioni nane ili kufanikisha shoo hiyo ambayo ilikamilika siku ya Ijumaa.

Butita ambaye ndiye aliyeandika na kuelekeza shoo hiyo alisema kwamba pesa zile zilikuwa za kukimu mahitaji kama chakula, utengenezaji filamu, usafirishaji, mishahara kati ya mahitaji mengine.

"Kijana ametapika pesa. Hapo hajatumia chini ya milioni kama nane hivi kuendelea. Pia milioni zangu 3.5 ziko pale ndani" Butita alifichua.

Alipoulizwa kwa nini shoo ile ilichukua muda mfupi tu ilhali pesa nyingi zilitumika Butita alieleza kuwa ilikuwa ghali  mno kuifanikisha.

"Tuligundua kuwa tukikaa na wasichana kama siku saba inakuwa ngumu kwetu kwa upande wa pesa na wakati. Kwa mfano mimi sijalala poa. Niko na usingizi sana, wakatimwingine tulikuwa tunalala saa kumi asubuhi. Kuna vitu natahariri usiku . Tunawapatia vipindi vitatu ama vinne, nyinyi mnaona nne pekee lakini sisi tumechoka na hao wasichana siku kama saba. Nahisi shoo hiyo inahitaji siku zaidi. Kam ishirini na moja hivi" Butita alisema.

Mchekeshaji huyo pia  alisema kwamba alikuwa ameonya Omondi dhidi ya kununua nyumba ambayo inadaiwa kumgharimu milioni 141.

"Nilimwambia ile pesa tuende tununue shamba tutengeneze kitu mzuri, tutengeneze. Tufanye biashara nzuri. Nilimwambia kutengeneza nyumba ni kukosa mwelekeo." Alisema Butita.