Kweli ama kiki tu? Manzi wa Kibera atengana na mumewe wiki mbili tu baada ya kufunga ndoa

Muhtasari

•Matendo ya wanandoa hao wawili  ya hivi karibuni katika kurasa zao za Instagram yameonyesha wazi kwamba huenda kitumbua kimeingia mchanga

•Obidan alidai kwamba ndoa kashfa huku akishauri wale ambao hawajafunga ndoa dhidi ya kuchukua hatua hiyo

Image: HISANI

Huenda ndoa kati ya mwanasoshalaiti Manzi wa Kibera na mcheshi Obidan Dela imegonga mwamba takriban wiki mbili baada yao kufunga pingu za maisha.

Matendo ya wanandoa hao wawili ya hivi karibuni kwenye mtandao wa Instagram yameashiria wazi kwamba huenda tayari kitumbua kimeingia mchanga.

Siku ya Jumanne mwanasoshalaiti huyo mzaliwa wa Kibra alipakia video iliyoonyesha moyo ambao umevunjika mara mbili na kuiambatanisha na emoji za kilio.

Manzi wa Kibera aliendelea kueleza kuwa  hawezi endelea kuvumilia tena  kwani kwa muda sasa hajakuwa na raha.

"Siwezi shikilia zaidi.. sijakuwa na furaha" Manzi wa Kibera aliandika.

Mwanasoshalaiti huyo alieleza hisia zake kupitia maneno ya wimbo Blu Cantrell 'Breathe' yanayosema kuwa mapenzi yanapoumiza na kuonekana kama kwamba hayatafanikiwa basi ni heri kujipatia nafasi ya pekee ili kila mmoja apate kupumzika.

"Mapenzi yanapoumiza na kuonekana kama hayatafanikiwa. Labda kila mtu anahitaji muda pekee yake ili tupumue " Manzi wa Kibera alieleza kwa maneno ya wimbo.

Kwa upande wake Obidan alidai kwamba ndoa kashfa huku akishauri wale ambao hawajafunga ndoa dhidi ya kuchukua hatua hiyo.

"Ndoa ni kashfa, acha tuangazie mambo muhimu zaidi. Kama bado hujaoa kitu naweza kuambia ni unaweza fanya kitu ya maana na maisha yako ukiwa single" Obidan aliandika kwenye ukurasa wake wa Instagram. 

Wawili hao walifunga ndoa takriban wiki mbili zilizopita katika hafla iliyokuwa imepambwa kweli na kuhudhuriwa na watu wachache.

"Ndoto yangu ya kuwa mke ilitimia kwa harusi maridadi na familia. Shukran @chaliwakibera kwa kila kitu lakini hapa ndipo nasema kwaheri kwa mitaa" Manzi wa Kibera alitangaza kwenye mitandao ya kijamii.