"Siwezi kataza mwanangu kuoa mwanamke aliyemzidi umri" Nyota Ndogo atoa masharti ya mkaza mwana wake

Muhtasari

•Mama huyo wa watoto wawili amedai kwamba hawezi kuwa na tatizo lolote kuhusu pengo la umri kati ya mwanawe na mke anayetazamia kuoa bora tu hajatimia umri wa kutozaa kwani anatumai kupata wajukuu siku za usoni.

Image: INSTAGRAM// NYOTA NDOGO

Mwanamuziki mashuhuri nchini Mwanaisha Abdalla almaarufu kama Nyota Ndogo ameweka wazi kwamba hawezi kuwa na shida yoyote iwapo mwanawe anaweza fanya uamuzi wa kuoa mke aliyempiku kwa umri.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, mzaliwa huyo wa Pwani amesema kwamba amempatia mwanawe ruhusa ya kuoa mwanamke aliyemshinda umri ila kwa masharti.

Mama huyo wa watoto wawili amedai kwamba hawezi kuwa na tatizo lolote kuhusu pengo la umri kati ya mwanawe na mke anayetazamia kuoa bora tu hajatimia umri wa kutozaa kwani anatumai kupata wajukuu siku za usoni.

"Siwezi kumkataza mwanangu kuoa mwanamke aliyemzidi umri. Huo ni uamuzi wake. Muhimu awe hajafika menopause maana natakka kuona wajukuu zangu Inshallah" Nyota Ndogo alisema.

Msanii huyo ambaye amekuwa kwenye taaluma ya muziki kwa takriban miongo miwili ni mama ya watoto wawili, mmoja wa kiume anayejulikana kama Mbarak na mwingine wa kike anayeitwa Barke.

Nyota Ndogo alifunga pingu za maisha na mzungu kutoka Uholanzi anayejulikana kama Henning Nielsen miaka tano iliyopita ila hawajapata mtoto pamoja.

Wawili hao wamekuwa wakivuma kwa kipindi kirefu mwaka huu kufuatia drama ambazo zimesheheni ndoa yao tangu mwezi wa Februari.