"Ulinikubali jinsi tu nilivyokuwa" Vera amlimbikizia sifa Mauzo tele baada ya kuruhusiwa kutoka hospitali

Muhtasari

•Mwanasoshalaiti huyo mwenye umri wa miaka 32 alichukuliwa hospitalini na mumewe Brown Mauzo kwa gari aina ya Limousine siku ya Jumanne.

•Mama huyo wa mtoto mmoja alikumbuka mahusiano yake mabaya ya hapo awali na jinsi alivyohangaika huku akimshukuru Maulana kwa kumjalia mume wa ndoto zake.

Image: INSTAGRAM // VERA SIDIKA

Hatimaye mwanasoshalaiti mashuhuri Veronica Mungasia almaarufu kama Vera Sidika amepewa ruhusa kutoka hospitalini baada ya kujifungua mtoto wa kike wiki moja iliyopita.

Mwanasoshalaiti huyo mwenye umri wa miaka 32 alichukuliwa hospitalini na mumewe Brown Mauzo kwa gari aina ya Limousine siku ya Jumanne.

Vera ambaye alionekana kajawa na bashasha alimbubujikia sifa tele mwanamuziki huyo ambaye wamekuwa kwa ndoa kwa kipindi cha mwaka mmoja sasa.

"Imekuwa wakati mzuri. Tunapojipanga kutoka hospitalini kuelekea nyumbani na  @princess_asiabrown nilihisi kushukuru mpenzi wangu @brownmauzo254. Hata sijui nianze wapi" Vera aliandika kwenye ukurasa wake wa Instagram.

Mama huyo wa mtoto mmoja alikumbuka mahusiano yake mabaya ya hapo awali na jinsi alivyohangaika huku akimshukuru Maulana kwa kumjalia mume wa ndoto zake.

Aliridhishwa sana na kitendo cha Mauzo kumkubali kama mke wake akiwa jinsi tu pamoja na udhaifu wake na kumuwezesha awe mtu bora.

"Ninapotazama mahali tulikotoka, nakumbuka mahusiano yangu ya awali na nasema kweli Mungu ako na sababu kwa nini mambo mengine hukosa kufanikiwa. Alijua wewe ndiye mume anayenifaa ndio maana alihifadhi mazuri mwishoni. Ulijua nguvu na udhaifu  na ukanikubali jinsi tu nilivyo. Huwa unaniwezesha kuwa mtu bora" Vera alisema.

Mwanasoshalaiti  huyo aliendelea kusema kuwa binti yake ana bahati sana kuwa na baba bora zadi duniani.