"Iliniuma sana!" Shaniqwa asimulia jinsi mkewe alimuacha na kunyakuliwa na jamaa mwingine

Muhtasari

•Mwigizaji huyo alifichua kwamba shida zilianza kumuandama  baada yake kupoteza kazi ya utangazaji katika stesheni ya KTN.

•Shaniqwa alisema kuwa shida nyingi pale nyumbani zilimfanya mkewe aanze kucheza karata nje na ilimchukua muda kuthibitisha kuwa alikuwa amenyakuliwa na jamaa mwingine

•Mwigizaji huyo aliweka wazi kuwa kwa kipindi cha miezi saba ambayo imepita amekuwa akiishi na mwanawe ilhali aliyekuwa mke wake hajawahi enda kumuona tangu alipomuachia mtoto yule.

Image: HISANI

Mwigizaji na mcheshi Kelvin Mwangi almaarufu kama Shaniqwa amedhihirisha wazi kwamba ndoa yake na aliyekuwa mpenzi wake Naomi Jemutai ilivunjika mwaka uliopita.

Alipokuwa kwenye mahojiano na Jeff Kuria, mwigizaji huyo alifichua kwamba shida zilianza kumuandama  baada yake kupoteza kazi ya utangazaji katika stesheni ya KTN. 

"Mambo iliharibika zaidi. Mali yangu ikaanza kupigwa mnada na maajenti wa nyumba.. kuna rafiki yangu alikuwa anatoka Dubai nikamuomba 'lift'. Nikafahamisha mama yangu kwamba ningepeleka familia yangu nyumbani akakubali. Nilijaribu kufanya kazi zangu pale nyumbani lakini mambo hayakuenda vizuri. Nilikuwa napata kazi kidogo za kutangaza zinanisukuma kidogo.. rafiki yangu mmoja akaniambia nitoe familia yangu nyumbani niirejeshe Nairobi ili mke wangu asake kazi" Shaniqwa alisimulia.

Alisema kuwa mkewe alibahatika kupata kazi katika duka la kuuza simu na baada ya miezi kadhaa wakahamia katika nyumba ya kukodisha.

Shaniqwa alisema kuwa shida nyingi pale nyumbani zilimfanya mkewe aanze kucheza karata nje na ilimchukua muda kuthibitisha kuwa alikuwa amenyakuliwa na jamaa mwingine.

"Mke wangu alianza kunicheza. Angepatiwa ruhusa ya kupumzika nyumbani kisha aniache na mtoto  alafu aende kwa jamaa huyo. Nakumbuka siku moja ilikuwa siku ya kuadhimisha kuzaliwa kwa mtoto wetu, hakutaka kuja alitaka kuenda kwa jamaa huyo. Nilikuwa nafahamu ila sikuwa na uhakika. Ningemwambia aende achukue mtoto kwa kuwa nachelewa kisha aanze kulalamika. Vita ikaanza pale nyumbani, hadi nikaenda kujificha kwa rafiki yangu siku mbili. Niliporudi aliniambia pale ni kwake nirudi mahali nilikokuwa nakaa. Hapo watu wakaanza kunitumia picha kwenye mtandao wa Instagram. Wakaanza kuuliza kwani tulikosana na mke wangu kwa kuwa alikuwa anaishi na jamaa mwingine

Kidogo kidogo nikapigiwa na mpenzi wa jamaa huyo akaniambia kwamba aliona mke wangu akiwa amepigwa  picha akiwa amevaa nguo ambazo alikuwa ameacha kwa mpenzi wake. Kidogo kidogo nikatumiwa picha wakiwa wanabusu na jamaa yule" Alisimulia

Alisema kuwa alisikitika zaidi usiku mmoja alipoamka na kupata mkewe akizungumza na jamaa aliyekuwa anachumbiana naye na hapo ndipo akaamua kumfukuza.

"Tulikosana, akachukua mtoto akaenda kwa jamaa huyo maeneo ya Ruiru. Nilipata kama amefunga nyumba na kuniachia funguo. Usiku huo sikuweza kulala, nilihisi kama kwamba nitakufa" Alisimulia Shaniqwa.

Mwigizaji huyo alisema kuwa jambo hilo lilimuumiza sana hadi akaanza kupatwa na msongo wa mawazo ambao ulifanya afya yake idhoofike.

Alisema kuwa baada ya miezi kadhaa mkewe alirejea nyumbani baada ya kutemwa na jamaa aliyekuwa anachumbia ila wakakosana tena baada ya siku mbili tu.

"Alikasirika baada ya kuchukua simu yangu na kupata kuwa tulikuwa tunamzungumzia na baadhi ya marafiki wangu ambao walikuwa wamenisaidia wakati nilikuwa na shida. Nilifaa kueleza marafiki hao sababu zangu kumrejesha nyumbani kwani walikuwa wamefukuzwa mahali walipokuwa wameenda" Alisema.

Baada ya takriban miezi miwili mkewe alimpelekea mtoto akidai kwamba alitaka kuenda kazi mahali hakuwahi mchukua tena.

"Alinitumia ujumbe kwamba ningeendelea kuishi na mtoto yule.. Mtoto huyo alikuwa ameletwa pale nyumbani na nguo tatu, nne hivi na kiatu moja.. nikapigia marafiki wangu ambao walikuwa wamenisaidia. Wakakubali kutusaidia ila wakanionya nisiwahi rudiana na mwanadada huyo" Alisema.

Mwigizaji huyo aliweka wazi kuwa kwa kipindi cha miezi saba ambayo imepita amekuwa akiishi na mwanawe ilhali aliyekuwa mke wake hajawahi enda kumuona tangu alipomuachia mtoto yule.